Latra wazungumzia mabadiliko njia za daladala Dar

Muktasari:

Baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto wanazopitia mara baada ya mabadiliko ya njia za daladala, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetoa ufafanuzi juu ya mabadiliko ya njia za daladala katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam huku sababu moja wapo ikiwa ni kukua kwa mji na watu kuongezeka.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) nchini Tanzania imesema mabadiliko ya njia (routes) za daladala katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yamefanyika kutokana na kukua kwa mji na watu kuongezeka.

Latra wamesema hayo baada ya wananchi kueleza changamoto wanazopitia mara baada ya mabadiliko hayo ikiwamo kuchelewa kufika kazini na kurudi majumbani hasa nyakati za asubuhi na jioni kutokana na kukaa kituoni kwa muda mrefu kusubiri daladala.

Ofisa leseni Latra Habiba Chambali amesema mamlaka inafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi hawaathiriwi na mabadiliko hayo kwa kuongeza idadi ya magari katika maeneo mbalimbali ya mji.

Baadhi ya njia zilizokumbwa na mabadiliko hayo ni zile zenye magari yanayofanya safari zake Buguruni- Masaki, Buguruni – Msasani, Rozana- Mbagala ambazo kwa sasa zinaanzia safari zao Temeke kupitia Buguruni na zile zilizokuwa zinatoka Rozana- Mbagala zinakwenda hadi Mbagala Magengeni.

”Kuna maeneo ambayo yalikuwa nje ya mji sasa yameendelea kwa hiyo ili tuweze kuwafikia wananchi wote ni lazima tuwapelekee magari hivyo tumeamua maeneo ya mjini yawe kwa ajili ya kushusha na kupakia, ila gari zinaanzia yale maeneo ya pembezoni ambako gari ni chache,” amesema ofisa leseni huyo wa Latra.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ambayo mji unakuwa hawatoi nauli mara mbili kutokana na hali ya uchumi iliyopo hivi sasa.

”Zamani kulikuwa na gari zinatoka Buguruni kwenda Mnazi mmoja tumezitoa hizi gari na kuacha maeneo haya kuwa sehemu ya kupakia na kushusha na hakuna mwananchi anayelipa nauli mara mbili kwa hawa ambao wapo mjini kuna gari zaidi ya 2000 zinapita Buguruni kwenda maeneo mbalimbali ya mji,” amesema  

Amesema jinsi alivyoathiriwa na mabadiliko hayo, mkazi wa Ilala Munira Ismail amesema zamani alikuwa akipanda gari  Buguruni mpaka Masaki lakini changamoto iliyopo sasa ni kwamba gari zote ambazo zilikuwa zinaanzia Buguruni zimehamishiwa Temeke, akisema kuwa zinachelewa kufika na zinafika zikiwa zimejaa.

”Mimi naona kuhamisha gari siyo suluhisho bali kama huko wanakozipeleka wameona kuna umuhimu sana wangetubakishia chache ili kutuwahisha kazini asubuhi,” amesema.

Mkazi mwingine wa Ilala Juma Hassani amesema kubadilishwa kwa njia hizo kumebadilisha pia ratiba yake ya kwenda kazini kwa kile alichodai kuwa magari yamekuwa yakipatikana kwa shida.