Lema, Mnyika, Sugu wavaa magwanda ya Chadema maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru

Monday December 9 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Wamepigia gwanda bwana! Kama viongozi na wanachama wa chama tawala cha CCM nchini Tanzania walidhani ni wao tu watatinga uwanjani kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru jijini Mwanza wakiwa wametinga sare rasmi za chama chao, basi wamekosea.

Chadema ambao nao wametinga uwanja wa CCM Kirumba leo Jumatatu Desemba 9, 2019 inakofanyika maadhimisho hayo ya Kitaifa wakiwa ndani magwanda ambayo ni miongoni mwa mavazi rasmi ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Kama walivyo viongozi wa CCM waliokaa jukwaa kuu, viongozi wa Chadema ambao wanaongozwa na Mwenyekiti wao Taifa, Freeman Mbowe kuhudhuria maadhimisho hayo nao wametinga magwanda. Mbowe yeye amevaa suti nyeusi na shati jeupe.

Wabunge wa Chadema walioketi jukwaa kuu wakiwa wamevaa magwanda Godbless Lema (Arusha Mjini), John Mnyika (Kibamba), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini) pamoja na Meya wa Ubungo, Dar es Salaam Boniface Jacob.

Wabunge hao wameketi eneo moja na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria na mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Advertisement

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Advertisement