Lema amlipua Dk Kigwangala bungeni

Wednesday April 15 2020

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amemshukia  Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangala kwamba anadhalilisha watu bila sababu za msingi huku akishinda kwenye mitandao ya kijamii.

Lema ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 15, 2020 bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akichangia hoja hotuba ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, iliyowasilishwa  Waziri, George Mkuchika.

Lema amesema kuna baadhi ya viongozi wanajifanya miungu watu, wanashindwa hata kufahamu mipaka yao ya madaraka na kusababisha malalamiko mengi kwa wananchi.

Amesema imefikia hatua hata wananchi  wanakoseshwa haki zao kwa hofu ya viongozi.

Ametolea mfano kitendo cha kuwarusha kichura watumishi wa Maliasili kilichofanywa na Dk Kigwangala alipokwenda kuwavisha nishani.

Lema amesema kitendo kile kiliwadhalilisha watumishi hao ambao waliambatana na ndugu jamaa, watoto kushuhudia kutunukiwa kwao nishani.

Advertisement

 

 “Lakini pia wapo viongozi wengine wana mapungufu yao, mfano mzuri ni hivi karibuni pale Arusha, Kaimu Mkurugenzi alikamatwa na polisi, lakini Mkuu wa wilaya na DSO walipokwenda kumwekea dhamana, OCD (mkuu wa polisi wilaya) aliwagomea. Hebu fikiria kama mkuu wa wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi anagomewa na OCD, sembuse raia wa kawaida,” amesema Lema.

Katika hatua nyingine mbunge huyo amesema ameamua kuwa kimya kwa mambo mengi ambayo yanafanyika mkoani kwake kwa sababu anataka kupita kwa urahisi katika uchaguzi mkuu ujao hivyo hawezi kuchangia mambo mengi.

Hata hivyo, amempongeza Waziri Mkuchika kwa kauli zake za makatazo na kukemea pale viongozi wanapo potoka.

Lakini ameiomba serikali kumuunga mkono ili kukomesha hali hiyo inayoonekana kuota mizizi.

Advertisement