Lema ashikiliwa na polisi mkoani Singida

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

Singida. Jeshi la Polisi mkoani Singida nchini Tanzania linamshikilia Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kwa tuhuma ya upotoshaji wenye lengo la kulichonganisha jeshi hilo na wananchi.
Februari 29 mwaka huu, Lema akiwa katika mazishi ya Katibu wa Chadema jimbo la Manyoni Mashariki, Alex Joas alitaja orodha ya watu 14 waliouawa kwa kuchinjwa na kuchomwa moto wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake leo Jumanne Machi 3 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike amesema mtuhumiwa Lema amekamatwa jana jioni mjini Arusha na kisha kusafirishwa hadi Singida mjini.
Amesema hivi karibuni Lema alipokwenda Manyoni kuhudhuria mazishi ya dereva wa boda boda Alex Joas alitumia fursa hiyo kupotosha wananchi.
Njewike amesema Lema alitoa taarifa ya upotoshaji, kwamba  Jeshi la Polisi halikuchukua hatua zo zote dhidi ya matukio ya mauaji ya wakazi 14 Wilaya ya Manyoni.
Amesema mauaji ya watu hao 14 ambayo yalitokea kati ya Agosti mwaka jana hadi Machi mwaka huu yote wameyafanyia kazi na mengi yamesababishwa na wivu wa mapenzi.
“Moja kuna mama aliua mtoto wake wa miezi miwili baada ya baba wa mtoto huyo, kutelekeza familia. Watuhumiwa wa mauaji hayo, karibu wote kesi zao zipo mahakamani. Wengine wapo mahabusu. Kasoro watuhumiwa wawili tu, ambao bado tunaendelea kuwasaka,” amesema.
Njewike amesema Lema atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.