Lema asimulia kilichomkuta kuingia anga za DC Sabaya

Moshi. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesimulia kilichomtokea wilayani Hai hadi kukamatwa na polisi, akibainisha kuwa hahitaji kibali kwenda eneo lolote nchini.

Lema ameenda mbali na kudai aligoma gari yake kupekuliwa na polisi akihofia kubambikiwa kesi hadi mkuu wa upelelezi mkoa (RCO) wa Kilimanjaro, Dotto Mdoe alipofika kituoni.

Lema na mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu walikamatwa juzi kwa amri ya mkuu wa wilaya hiyo, Lengai ole Sabaya aliyewatuhumu kufanya vikao vya siri ili kuibua taharuki kwa wananchi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema alikamatwa alipofikishwa kituoni, mkuu wa polisi wilaya ya Hai (OCD), Lwewe Mpina alimhoji sababu za kuingia Hai bila kibali chake.

“Nilikwenda mwenyewe baada ya kuambiwa natafutwa baada ya Helga kukamatwa. Nilifika nikaingia kwa OCD na kujitambulisha akaniambia kaa chini,” alidai Lema na kuongeza:

“Nilimwambia siwezi kukaa chini. Nikamwambia anieleze kosa langu akasisitiza nikae chini. Nikamwambia siyo kukaa chini tu. Nikalala kwa tumbo. Akaniweka mahabusu.

“Baada ya muda kupita akaniita akinihoji kwa nini nimekuja Hai bila kibali chake. Nikamwambia mimi ni Mtanzania sihitaji Passport (hati) ya kusafiria kwenda eneo lolote la Tanzania,” alisema.

Alisema katika majibizano hayo alilazimika kutumia lugha ya kuudhi dhidi ya OCD, kwa kuwa alimuona kama Polisi asiyeelewa majukumu yake.

“Baada ya RCO kuja aliulizwa kosa la Lema ni nini akaendelea kusisitiza nimekuja Hai bila kibali chake. Baadaye ikaonekana si kosa nikahojiwa kwa kumtukana OCD,” alisema.

Alikanusha madai ya Sabaya kuwa walifanya kusanyiko lisilo halali na kwamba, alikwenda kufuatilia tukio la katibu mwenezi wa Hai, Humphrey Swai kutekwa na wasiojulikana.

“Walimteka wakamlazimisha asome waraka kuwa Chadema Hai wao watashiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hili ndiyo lilinileta kama mjumbe wa Kamati Kuu,” alisema Lema.

Alisema baada ya katibu huyo kurekodiwa na mmoja wa waandishi wa TV mmoja ya mtandaoni, video hiyo ilirushwa Youtube lakini iliondolewa na kuomba radhi.

Juzi, Sabaya alieleza sababu za kuamuru Lema na Helga wakamatwe kuwa ni kutokana na kuingia Hai na kufanya mikusanyiko isiyo halali kwa lengo la kuzusha taharuki kwa wananchi.

“Tumemkamata mwenyekiti na wengine wawili lakini Lema alifanikiwa kutoroka kupitia mlango wa nyuma na kutelekeza gari lake aina ya Toyota Land Cruiser,” alisema Sabaya na kuongeza:

“Kitendo cha Lema kutoka Arusha kuja Hai kufanya vikao vya siri ni sawa na kuvuka msitari mwekundu hili hatuwezi kulivumilia. Namtaka Lema ajisalimishe mwenyewe polisi.”

Muda mfupi baada ya Sabaya kutoa kauli hiyo, Lema aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa amesikia anatafutwa na polisi na anakwenda mwenyewe kituo cha Polisi Hai.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni alipoulizwa jana, alisema hakuwa na taarifa hizo.