Lipumba: Kifo cha Khalifa ni pengo kubwa CUF

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kifo cha katibu  mkuu wa chama hicho, Khalifa Suleiman Khalifa kimeacha pengo kubwa katika chama hicho.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kifo cha katibu  mkuu wa chama hicho, Khalifa Suleiman Khalifa kimeacha pengo kubwa katika chama hicho.

 

Khalifa ambaye amewahi kuwa mbunge wa Gando kuanzia mwaka 1995  hadi 2015 amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Machi 31, 2020  katika hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

Profesa Lipumba ameeleza hayo leo Jumanne Machi 31, 2020 wakati akizungumza na Mwananchi.

 

Amesema  kifo cha mwanasiasa huyo na mtendaji mkuu wa chama hicho ni pigo kubwa.

 

"Msiba mzito kwetu tumepokea salamu nyingi za rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa akiwemo Rais John Magufuli ambaye ametoa pole kwa familia na chama cha CUF. Katika salamu zake Rais Magufuli amesema   wamefahamiana na Khalifa tangu mwaka 1995 wakiingia Bungeni kwa mara ya kwanza."

 

"Rais Magufuli ameniambia  Khalifa alikuwa rafiki yake tangu wakati huo," amesema Profesa Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.

 

Profesa Lipumba amesema Khalifa alikuwa nguzo muhimu na mzoefu katika siasa za Zanzibar na Tanzania bara, kifo chake ni pigo kubwa kwa wanachama wa chama hicho.

 

"Khalifa alikuwa mzalendo, mwenye mapenzi na wananchi wote na alikuwa mzoefu kwenye masuala ya siasa za Tanzania na Tanzania bara," amesema Profesa Lipumba kwa sauti ya upole.

 

Machi 16, 2019  Khalifa akichaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF lkuwa katibu mkuu wa pili wa chama hicho akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alivuliwa uanachama

Khalifa atazikwa  leo saa 7 mchana katika makaburi ya Kisutu wilayani Ilala.