VIDEO: Lissu, Kubenea kugombea umakamu mwenyekiti Chadema

Muktasari:

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea wamejitosa kugombea umakamu mwenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Desemba 18, 2019.


Arusha. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea wamejitosa kugombea umakamu mwenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Desemba 18, 2019.

Leo Jumamosi Novemba 30, 2019 katika mkutano wa uchaguzi wa viongozi kanda ya Kaskazini mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema alimuomba Lissu kugombea nafasi hiyo na amekubali.

“Nimemuomba na amekubali alisaini fomu jana jijini Nairobi, Kenya,” amesema Mbowe na kuwataka wagombea wengine kuwa na nidhamu ya uongozi, kuacha kutoa lugha chafu mitandaoni.

"Nilikusudia kutokuwa kiongozi Chadema, si kwa woga bali dhamira ya kuwapa wengine nafasi ya kugombea kama sheria na katiba ya chama inavyosema lakini wameniomba kuwa mwenyekiti tena,” amesema Mbowe.

Mbowe aligusia baadhi ya wanachama wa chama hicho kuhama, wakiwemo madiwani na kusema kila mtu ana udhaifu wake,  si kila mtu anaweza kuvumilia mikikimikiki ya upinzani.

Kwa upande wake Kubenea amelieleza Mwananchi kwamba amerejesha fomu kuwania nafasi hiyo huku akisisitiza kuwa amejipanga kushinda.