Lissu: Marafiki wataamua hatima yangu kurejea Tanzania

Muktasari:

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atarejea Tanzania baada ya  marafiki zake kumhakikishia usalama wake.


Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atarejea Tanzania baada ya  marafiki zake kumhakikishia usalama wake.

Lissu ametoa kauli hiyo jana Alhamisi Novemba 28, 2019  katika mahojiano na kituo cha televisheni cha KTN cha nchini Kenya baada ya kuulizwa swali na mtangazaji Paul Nabiso kuhusu mpango wake wa kurejea nchini baada ya kumaliza matibabu.

Mwanasheria mkuu huyo wa Chadema amesema, “hali ya usalama wangu bado si nzuri, nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani kesho na keshokutwa ninapigwa risasi tena. Bado kuna vitisho vya aina hii,  watu wenye busara lazima wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama.”

“Hizi jitihada zinafanywa na marafiki wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha nakuwa salama kurudi Tanzania. Ikifika mahala wakasema usalama wangu utaangaliwa nitarudi nyumbani.”

“Sitaki kuishi uhamishoni na sipo uhamishoni. Nilienda kwenye matibabu nimeshatibiwa nasubiri niambiwe usalama wangu utakuwaje katika mazingira halisi.”

Oktoba 9, 2019 wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA), Lissu alisema kuwa hawezi kurejea Tanzania kwa kuwa mazingira ya  usalama wake si mazuri.

Septemba 7, 2019,  Lissu alikaririwa akisema atarejea Tanzania “mchana kweupe” akitokea Ubelgiji alikoenda kutibiwa, kwamba suala hilo halitakuwa siri kama ambavyo anashauriwa na watu wengi.

Katika mahojiano ya jana, Lissu amesema, “tunazungumzia mtu ambaye amepigwa risasi 16, amefanyiwa operesheni 24 katika kipindi cha miaka miwili. Ni makosa kiasi gani kuuliza mtu aliyefanyiwa hivi na watu ambao hawajakamatwa mpaka leo akirudi atakuwa salama au la, ni makosa kiasi gani kuuliza swali kama hilo.”

Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa Ubelgiji kukamilisha matibabu na sasa amepona.

Katika mahojiano hayo ya dakika 28, Lissu aliwashukuru wananchi wa Kenya kwa kumchangia damu alipopigwa risasi na kugusia ushirikiano alioupata kutoka kwa mashirika mbalimbali kuhusu kurejea Tanzania.

“Nimewasiliana na mashirika mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu, kidemokrasia pia na Serikali za nchi kadhaa. Jitihada ni kubwa kuhakikisha tunatengeza mazingira salama ya mimi kurudi nyumbani.”

“Nililetwa hapa (Nairobi) nikiwa sijitambui Wakenya walijitolea damu yao ili kuokoa maisha yangu, mimi ni Mkenya pengine sina hati ya kusafiria ya Kenya lakini nina damu ya kutosha ya Kenya ya kunifanya niwe Mkenya. Nimekuja hizi siku mbili kuwapa shukrani wananchi wa Kenya, madaktari, manesi na marafiki waliokuja wakati mbaya kwangu, ninawaeleza kuwa nimepona na yote waliyojitolea hayakuenda  bure.”