Lissu: Msichague viongozi wasaka fedha

Muktasari:

Mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu amewataka Watanzania kuchagua viongozi ambao hawatakwenda kwenye mabaraza ya madiwani na bungeni kusaka fedha.

Handeni. Mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu amewataka Watanzania kuchagua viongozi ambao hawatakwenda kwenye mabaraza ya madiwani na bungeni kusaka fedha.

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema ameeleza hayo leo Jumatatu Oktoba 26, 2020 katika mkutano wa kampeni jimbo la Handeni mkoani Tanga.

Uchaguzi mkuu wa Tanzania unafanyika Jumatano Oktoba 28, 2020 siku ambayo Lissu amewataka wananchi kutofanya makosa kwani uchaguzi ni mustakabali wa maisha yao.

Amesema baadhi ya wagombea hawafikirii kutetea maslahi ya waliowachagua wala kuihoji Serikali kwenye vyombo hivyo, bali wanaangalia namna ya kupata fedha.

“Hakikisheni Oktoba 28 hamuendi kufanya makosa kwa kuchagua viongozi wanaokwenda kutetea maslahi yao, awe kiongozi anayefikiria kuhusu wale waliomchagua msipofanya hivyo mnaweza kujutia,” amesema Lissu.

Alitumia mkutano huo kuwaahidi wakazi wa Handeni kwamba akiwa rais atafuatilia na kutafuta ufumbuzi wa mgodi wa Magambazi ili uendelee na kazi.