Lissu: Ninawaonea huruma wadhamini wa kesi yangu - VIDEO

Muktasari:

Makamu mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu amesema anawaonea huruma waliomdhamini katika kesi ya uchochezi inayomkabili, kuiomba mahakama itende haki kwa kuwa hawawezi kumrejesha Tanzania.

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu amesema anawaonea huruma waliomdhamini katika kesi ya uchochezi inayomkabili, kuiomba mahakama itende haki kwa kuwa hawawezi kumrejesha Tanzania.

Lissu ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji anakabiliwa na kesi ya uchochezi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi Januari 20, 2020 wadhamini wake walitakiwa na mahakama hiyo kuhakikisha anarejea nchini ili kuendelea na kesi yake.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki amesema wadhamini hao,  Robert Katula na Ibrahimu Ahmed  hawawezi kumrejesha Tanzania kwa kuwa hawakumpekea.

“Mimi nitarejea nitakapohakikishiwa usalama wangu, uhai ni mkubwa kuliko kesi hiyo,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

Lissu ameeleza hayo jana Jumanne Januari 21, 2020 ikiwa ni siku moja tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa siku 31 kwa wadhamini wake kuhakikisha wanamfikisha mahakamani hapo.

Juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilisikilizwa kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alielezwa na wadhamini wa Lissu kuwa wamemuandikia barua mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtaka amrejeshe mshtakiwa huyo nchini.

Lissu yupo Ubelgiji tangu Januari 6, 2018 alikokwenda kwa matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako nako alifikishwa usiku wa Septemba 7,  2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake eneo la Area D, Dodoma.

Hakimu Simba alitaka wadhamini hao kuhakikisha Februari 20 wanampeleka mshitakiwa hiyo na si vinginevyo. Kabla ya maagizo hayo Katula alisema juhudi walizofanya kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani ni pamoja na kumwandikia barua Mbowe.

Katika maelezo yake kuhusu wadhamini wake, Lissu amesema, “ninawahurumia sana wadhamini wangu kwa sababu wamewekwa katika mazingira ambayo ni magumu na mabaya bila sababu ya msingi.”

“Mtu anapokuwa mdhamini katika kesi za jinai, anachukua reasonable steps kuhakikisha mtu aliyemdhamini anafika mahakamani wakati anapohitajika kufika mahakamani.”

Ameongeza, “mdhamini sio askari magereza wa kumsimamia mtuhumiwa muda wote na huo siyo udhamini. Kazi ya mdhamini siyo kuhakikisha kwamba huyo aliyedhaminiwa anakuwa naye muda wote bali wajibu wake ni kuhakikisha anafika mahakamani kwa kuchukua reasonable steps.”

“Kwa mfano mtuhumiwa amekimbia au ametoroka, anachotakiwa kufanya mdhamini ni kwenda mahakamani na kusema niliyemdhamini ametoroka na nimemfuatilia na kushindwa kumpata na siwezi kumpata na akifanya hivyo mahakama inamfutia huo udhamini na hiyo ndiyo sheria ya Tanzania.”

Huku akizungumza kwa umakini Lissu amesema, “katika kesi yangu, hakimu anajua na waendesha mashtaka wanajua kuwa niliondoka Tanzania katika mazingira gani, wote wanajua na dunia inajua, katika mazingira hayo hata bila kuambiwa au kuombwa alipaswa awaondoe kwa sababu hawana namna yoyote ya kunirudisha.”

“Sasa  mahakama huyu Hakimu Simba anasema wanipeleke mahakamani, hawawezi kunileta na hawawezi tena na wamesema hivyo na Hakimu Simba anachokifanya anacheza ngoma ambayo haipo kisheria.”

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh. Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam ambapo Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’ Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.