Lissu, vigogo Chadema wakutana Kenya

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu inasemekana amekutana na vigogo wa chama hicho katika kikao kilichofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, Mwananchi limeelezwa.

Hakuna kiongozi wa Chadema aliyekuwa tayari kuthibitisha kikao hicho na Lissu inaaminika alikwenda Kenya akitokea Ubelgiji, ambako anaishi kwa sasa baada ya kupatiwa matibabu.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa waliokutana na Lissu walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na ilikuwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mara ya mwisho kamati kuu ya Chadema ilikutana Desemba 20, mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa Lissu baada ya kumalizika kwa kikao hicho, alirejea Ubelgiji ambako yupo tangu Januari 6, 2018 baada ya kupelekwa kwa ajili ya matibabu akitokea Nairobi, Kenya.

Lissu alipelekwa Nairobi Septemba 7, 2017 akitokea Hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa nje ya nyumba yake, muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge.

Lissu alichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu Desemba 18, mwaka jana kuwa makamu mwenyekiti. Aliwahutubia wajumbe wa mkutano huo kupitia video ya mtandao wa mawasiliano wa kijamii wa WhatsApp kisha akapigiwa kura zilizompa ushindi.

Licha ya Chadema kutotoa taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho, Mwananchi limethibitishiwa na viongozi wa juu wa chama hicho kufanyika kwa kikao hicho.

“Ni kweli tumefanya kikao cha Kamati Kuu Nairobi na Lissu alishiriki mwenyewe na baada ya kumaliza aliondoka kurudi Ubelgiji,” kilisema chanzo chetu.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa na Mwananchi alisema, “chama hakijafanya kikao cha Kamati Kuu tangu ilipokutana kwa mara ya mwisho Desemba 20, jijini Dar es Salaam kwa siku moja na vyombo vya habari vilitaarifiwa kama ilivyo ada ya chama kila Kamati Kuu inapokutana.”

Licha ya maelezo hayo ya Makene, lakini Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu aliweka picha aliyopiga akiwa na Lissu kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika, “Mjumbe wa Kamati Kuu akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa kwenye vikao vya kamati kuu hivi karibuni.”

Picha nyingine ilisambaa juzi jioni mitandaoni ikionyesha mandhari kama yaliyopigwa ya Sugu na Lissu, ila hii iliwaonyesha wajumbe wa Kamati Kuu ambao ni Lazaro Nyalandu, Lissu na Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje.

Pia ilikuwepo picha nyingine akiwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini.

Mwananchi lilipomtafuta Nusrat hakukubali wala kukana kuwapo kwa kikao hicho.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa kuhusu suala hilo alikanusha.

“Hizi taarifa umezitoa wapi mbona zinasambaa sana hakuna kikao cha kamati kuu kilichokaa Nairobi. Waulize hao waliopiga naye picha,” alisema.