Lissu achambua uamuzi wa mahakama kukataa maombi yake, asema atakata rufaa

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atakata rufaa kupinga Mahakama Kuu kukataa maombi yake ya kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.

 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atakata rufaa kupinga Mahakama Kuu kukataa maombi yake ya kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.

Leo Jumatatu Septemba 9, 2019 Jaji Sirillius Matupa amesoma uamuzi kuhusu maombi ya Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, akibainisha kuwa  hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Jaji huyo amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Kupitia mitandao ya kijamii, Lissu amesema amewasiliana na wakili wake, Peter Kibatala kuhusu uamuzi huo akidai  unaoonyesha kuwa mahakama ina hofu.

“Sisi hatukuwa na bado hatuna ugomvi na Tume ya Uchaguzi wala na Miraji Mtaturu (Mbunge wa sasa wa Singida Mashariki-CCM). Ukifungua kesi ya uchaguzi, kama anavyoshauri Jaji Matupa, unatakiwa kuthibitisha kwamba una 'cause of action', ugomvi na aliyechaguliwa au aliyesimamia uchaguzi,” amesema Lissu. 

Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliitisha uchaguzi kwa sababu iliandikiwa barua na Spika Job Ndugai kwamba kiti cha ubunge wa kipo wazi.

“Haijatukosea sisi na kwa sababu hiyo, hatuwezi kuishtaki kwa njia ya kesi ya uchaguzi. Miraji Mtaturu aligombea uchaguzi na kutangazwa 'mshindi' kwa sababu aliitikia wito wa Tume. Hajatukosea sisi na kwa sababu hiyo, hatuwezi kumshtaki kwa kutumia njia ya kesi ya uchaguzi,” ameeleza Lissu. 

Amesema aliyewakosea Spika Ndugai na 'dawa' stahiki kwa makosa yake sio kesi ya uchaguzi, bali ni marejeo ya kimahakama ya uamuzi wake.

“Hatukukosea chochote kufungua maombi ya marejeo ya kimahakama. Hoja ya kwamba kutakuwa na mgogoro wa kikatiba, wabunge wawili, ni hoja isiyokuwa na mantiki au maana yoyote.”

“Tulichoomba sisi ni Mahakama Kuu itamke kama uamuzi wa Spika Ndugai ulikuwa sahihi kisheria. Once (mara) Mahakama Kuu ikitamka kwamba uamuzi huo haukuwa sahihi kisheria, maana yake ni kwamba yote yaliyofanywa na Tume kufuatia uamuzi huo yalikuwa batili. Tunakwenda Mahakama ya Rufaa ya Tanzania,” amesema.

Lissu  aliyeko nchini Ubeligiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2017 alitangazwa kuvuliwa ubunge Juni 28, 2019 na Spika Ndugai.

 

Spika Ndugai alitoa sababu mbili za kufikia uamuzi huo kwanza ni kutokujaza fomu za mali na madeni kwa viongozi wa umma pamoja na kutotoa taarifa ya wapi alipo.