Lissu amesema hayatambui matokeo yanayoendelea kutangazwa na NEC

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu

Muktasari:

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu amesema hayatambui matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana Oktoba 28, 2020 ambayo yanaendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

 

 

Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu amesema hayatambui matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana Oktoba 28, 2020 yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Amesema hayatambui matokeo hayo kwa madai kuwa mawakala wa Chadema walinyimwa barua za utambulisho, kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura, baadhi ya matokeo kutobandikwa vituoni na kukosewa kwa utaratibu wa kujumlisha kura.

Hata hivyo, sababu zilizotolewa na Lissu zilijibiwa na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini jana, wengi wakieleza kuwa  kasoro nyingi zilijitokeza zilipatiwa ufumbuzi.

Kuanzia leo asubuhi Alhamisi Oktoba 29, 2020 NEC inatangaza matokeo ya urais inayopata kutoka majimboni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema, ameiomba jumuiya ya kimataifa kutoutambua uchaguzi huo.

"Kilichotokea jana si uchaguzi, kwa mujibu wa sheria za Tanzania  na taratibu za kimataifa. Hatuwezi kutambua kitu ambacho si uchaguzi.

Hatuwezi kutambua chochote. Hatukubaliani na matokeo yoyote," amesema Lissu.

Lissu, aliyeelezea mchakato wa uchaguzi tangu uteuzi wa wagombea, amesema chama chao kimejitahidi kutimiza wajibu wake.

"Ni Watanzania ndio walioibiwa haki yao, na tumesema katika kampeni, hatuwezi kukubali kuibiwa. Hivyo Watanzania ndio wana wajibu wa kutetea haki yao,” alisema mwanasheria huyo.

"Watanzania watumie hatima ya maisha yao kudai haki ya kidemokrasia. Sisi tumefanya upande wetu na Watanzania waliitikia, sasa wadai haki yao kwa namna yoyote. Kudai haki si kosa la jinai."

jumuiya ya kimataifa, Lissu amezitaka nchi jirani za bara la Afrika, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na taasisi za kimataifa zilizoleta waangalizi, kutotambua uchaguzi huo.

"Zisije zikatoa utambulisho au kukubaliana na hii kitu.  Tunaomba marafiki zetu wasiyatambue matokeo ya uchaguzi huu," amesema.

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa ina uwezo wa kusaidia Watanzania kudai haki zao za kidemokrasia.

Ametaja hatua zinazoweza kuchukuliwa na jumuiya hiyo kuwa pamoja na kuzuia viongozi na watendaji wa serikali kusafiri nje ya nchi, kufanya biashara za kimataifa na miamala.