Lissu kupiga kura kijijini kwake Singida

Mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu

Muktasari:

Mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu amesema atapiga kura katika kituo cha shule ya Msingi Tewa kilichopo  kijiji cha Mang’onyi mkoani Singida.

Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu amesema atapiga kura katika kituo cha shule ya Msingi Tewa kilichopo  kijiji cha Mang’onyi mkoani Singida.

Lissu ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 26, 2020 katika kijiji cha Mang’onyi wilayani Ikungi Mkoa wa Singida katika mkutano wake wa kampeni. Lissu atafanya mkutano wa mwisho wa kampeni kesho jijini Dar es Salaam.

“Nakuja kupiga kura Tewa shule ya msingi kituo namba A,” amesema Lissu huku akisisitiza suala hilo kwa lugha ya Kinyaturu.

“Ninachowaombeni ni kwamba kesho kutwa (Jumatano) tumalizane na CCM. Yaani wasitushinde kwenye kituo hata kimoja, hata kwenye kijiji hiki kimoja, wasitushinde hata kwenye kata,” amesema Lissu.

Aliwataka mawakala hao kuhakikisha kuwa wanalinda kura,“ hakikisheni kwamba tunawashinda...,tuwashinde katika kila kituo, kijiji na kata.”

Aliwataka wanachama wa chama hicho kuhakikisha kuwa mawakala wa Chadema wanakuwepo kila kituo ili shughuli ya kupiga kura iwe sawa.

Amesema uwepo wa wakala kwenye kituo ndio hutoa nafasi ya uwazi katika upigaji kura, kusisitiza kuwa suala hilo lazima litiliwe mkazo na kusimamiwa vilivyo.