VIDEO: Lugola amuonya Musiba, mwenyewe asema yupo tayari kukamatwa

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amemuonya  mwanaharakati, Cyprian Musiba akimtaka kuacha tabia ya kuwachafua viongozi na watu mbalimbali kwa madai kuwa ametumwa na Serikali.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amemuonya  mwanaharakati, Cyprian Musiba akimtaka kuacha tabia ya kuwachafua viongozi na watu mbalimbali kwa madai kuwa ametumwa na Serikali.

Wakati Lugola akisema hayo, Musiba amezungumza na Mwananchi na kusema yupo tayari kukamatwa, kuwekwa mahabusu au kufungwa jela lakini hatoacha kumsemea Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Lugola ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 13, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma, kusisitiza kuwa Musiba akiendelea atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri huyo amesema Musiba amekuwa akiwachafua baadhi ya viongozi na wananchi kwa madai kuwa ni mtetezi wa Rais Magufuli na kuwaaminisha watu kuwa anatumiwa na Serikali, jambo alilodai kuwa si kweli.

Lugola amesema Serikali haina mpango wa kuwatuma wanaharakati, haimtumii Musiba kuwaumiza watu akimtaka kufanya shughuli zake bila kutumia mgongo wa Serikali.

Amesema ikiwa ataendelea kuonyesha kuwa maneno yake yanawajengea hofu wananchi na anatumwa na Serikali, atachukuliwa hatua.

“Musiba asivuke mipaka ya harakati zake afanye shughuli alizoamua kuzifanya,” amesema Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara.

Alichojibu Musiba

Akizungumza na Mwananchi, Musiba amesema ameanza kuwa mwanaharakati miaka mitatu na nusu iliyopita, hajawahi kusema kama ametumwa na Serikali, CCM au Ikulu.

Amesema siku za hivi karibuni amewahi kuwataja baadhi ya viongozi na wabunge wa CCM katika mambo mbalimbali, wapo waliomuomba radhi Magufuli.

Amesema  kinachofanywa na Waziri huyo kinatokana na kuzoea kuona wanaharakati wanaotukana Serikali, “mimi situkani Serikali bali naisifia.”

“Aache (Lugola) kutumia Serikali kutaka kunidhibiti kwa sababu ni Waziri naamini nimezaliwa siku moja, nitakufa siku moja na hizo jela wameumbiwa watu. Kama anataka aje anikamate tu akaniweke, akanifunge, aje tu niko tayari hata sasa hivi, anipeleke mahabusu.”

Akizungumzia magazeti anayodaiwa kuyamiliki kutajwa kuchafua watu, Musiba amesema hawezi kuwa na chombo cha habari kinachoitukana Serikali kwa sababu anajitambua.

“Media zangu tunaandika vitu vizuri  tu kuhusu Serikali, yeye kama sehemu ya serikali sasa anataka kuniziba mdomo kisa nimetoa msaada jimboni kwake, sitakubali na hatoniziba mdomo, hawezi,” amesema Musiba.