Lukuvi akabidhi ekari 715 manispaa ya Kigamboni

Waziri wa Ardhi, Nyumba Maendeleo na Makazi, William Lukuvi akimkabidhi nyaraka mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni Ng'wilabuzu Ludigija.

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amekabidhi ekari 715 za ardhi kwa manispaa ya Kigamboni kama alivyoagizwa na Rais John Magufuli wiki iliyopita.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amekabidhi ekari 715 za ardhi kwa manispaa ya Kigamboni kama alivyoagizwa na Rais John Magufuli wiki iliyopita.

Februari 11, 2020 wakati akizindua ofisi za mkurugenzi na mkuu wa wilaya ya Kigamboni pamoja na hospitali ya wilaya hiyo, Rais Magufuli alimwagiza Lukuvi kuhamisha umiliki wa ekari hizo kutoka katika wizara yake kwenda kwa manispaa hiyo.

Leo Jumatatu Februari 17, 2020 , Lukuvi akiambatana na katibu mkuu wa wizara hiyo, Mary Makondo walikabidhi ekari hizo kwa viongozi wa wilaya na manispaa ya Kigamboni akiwamo mkuu wa wilaya hiyo, Sarah Msafiri.

"Leo nimetimiza maagizo ya Rais Magufuli ya kukabidhi ekari 715 mbele ya uongozi wa manispaa na wilaya ya Kigamboni. Natarajia kuona maeneo haya yanakuwa ya umma na sio kiwanja au makazi ya mtu mmoja moja," amesema Lukuvi.

Sarah amemshukuru Lukuvi kwa kutimiza ahadi hiyo na kuahidi kushirikiana na wizara hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ekari hizo walizokabidhiwa leo.