Lukuvi apiga marufuku maofisa ardhi kutoa ofa za viwanja

Tuesday October 22 2019

 

By Rajabu Athumani, Mwananchi [email protected]

Handeni. Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi amepiga marufuku maofisa ardhi kutoa ofa ya viwanja kuanzia leo Jumanne Oktoba 22, 2019.

Akizungumza leo na wananchi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga,  Lukuvi amesema kwa sasa hakuna ofa itakayotolewa na Serikali.

Lukuvi amesema madhara yaliyojitokeza katika kutoa ofa ni kufanyika udanganyifu kwa watumishi wasio waaminifu na kuisababishia Serikali hasara.

"Hakuna ofa nyingine ya ardhi ambayo Serikali itatoa. Waliopata ofa hao ndio wa mwisho maana ofa hizo zinasababisha magendo,” amesema waziri Lukuvi.

Pia, Lukuvi amesema masjala ya ardhi iliyokuwa mjini Moshi itahamia mkoani Tanga kwa sababu ni gharama kwa mwananchi kwenda Moshi kusaini hati kwa kuwa wengi hutumia gharama kubwa kufika katika mji huo wakati kiasi wanachotoa kwa ajili ya hati ni kidogo.

Lukuvi pia ameridhia kuanzishwa kwa baraza la ardhi Handeni baada ya kuonyeshwa jengo na kuridhika nalo.

Advertisement

Mkuu wa wilaya ya Handeni,  Godwin Gondwe amesema wilaya hiyo imeshaanza urasimishaji wa viwanja ili kupunguza migogoro, kubainisha kuwa viwanja 8,000 vimeshapimwa.

 

Advertisement