Lukuvi ataka Sh23 milioni za sherehe kuboresha mfumo wa kutoa huduma

Tuesday October 8 2019Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi

Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi amesema Sh23 milioni zilizokuwa zitumike katika maadhimisho ya siku ya Makazi Duniani kutumika kuboresha mfumo wa mapato na utoaji huduma za ardhi.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 8, 2019 imesema  Lukuvi ametaka maadhimisho ya mwaka 2019 kutofanyika sherehe na badala yake wananchi kufanya usafi katika maeneo ya miji wanayoishi.

“Maadhimisho ya mwaka huu zisifanyike sherehe na badala yake yatumike kutafakari kauli mbiu na kujipanga upya kutekeleza agizo la rais alilolitoa muda mrefu la kuwataka wananchi kujitolea kufanya kazi za usafi katika maeneo ya miji na wanayoishi.”

“Mamlaka za miji zina wajibu wa kukusanya taka kama mojawapo ya huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi na kwa upande mwingine wananchi wanao wajibu wa kulipia huduma hiyo kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mamlaka za mitaa,’’ imesema taarifa hiyo.

Lukuvi amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa taka sehemu ambazo hazistahili ili kupuka  athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuziba kwa mitaro ya maji ya mvua na mafuriko.

Advertisement

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Makazi Duniani (UN Habitat) kupitia azimio limetenga Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kuwa siku ya Makazi Duniani ambapo kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika jijini Nairobi, Kenya mwaka 1986.

Mwaka 2019 maadhimisho hayo yanafanyika kimataifa katika jiji la Younde Cameroon.

Advertisement