MABADILIKO: Iringa nao wamng’oa meya wao

Iringa. Wimbi la kung’oa mameya wa halmashauri jana lilihamia Iringa ambako baraza maalum la madiwani lilipiga kura ya kumuondoa Alex Kimbe ambaye baadaye aliiambia Mwananchi kuwa atakata rufaa kupinga uamuzi huo.

Huyo ni meya wa pili wa upinzani kung’olewa na baraza lake kwa staili hiyo ya uchunguzi wa tuhuma zake kufanywa na mkurugenzi na baadaye chombo hicho kupiga kura ya kumng’oa.

Wa kwanza alikuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam (Chadema), Isaya Mwita, ambaye pia jitihada zake za kutumia mahakama kuzuia kitendo hicho hazikufanikiwa.

Jana, ikiwa ni siku mbili baada ya mahakama kutupa maombi ya kuzuia mchakato wa kumng’oa Kimbe, kikao cha baraza hilo kiliitishwa jana na kufanikisha azma hiyo. Kikao cha 26 kiliahirishwa kutokana na akidi kutotimia.

Jana, wajumbe 14 ambao ni madiwani wa CCM walipiga kura kumng’oa Kimbe huku 12 wa Chadema wakiamua kutopiga kura.

Hata hivyo, Kimbe alisema kitendo hicho ni batili. Alisema waliopaswa kupiga kura kwa mujibu wa kanuni ni lazima wawe wajumbe 17 na si 14 na hivyo atakata rufaa kupinga uamuzi huo.

Mwishoni mwa Februari, mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Hamid Njovu aliwasilisha tuhuma nne dhidi ya Kimbe ambazo ni matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya rasilimali za halmashauri, mwenendo mbaya au ukosefu wa adabu na kushiriki katika vitendo vya rushwa.

Njovu alieleza kuwa tuhuma hizo zilitolewa na madiwani 19 ambao waliomba uitishwe mkutano maalum kupiga kura ya kutokuwa na imani na Kimbe ambaye alipewa barua na kutakiwa kujibu tuhuma hizo.

Kimbe hakutokea katika kikao ambacho alitakiwa kuhojiwa na kamati ya uchunguzi ya mkoa, jambo lililomfanya Njovu kuitisha mkutano maalum wa baraza Machi 26, lakini haukufanyika kutokana na kutotimia kwa akidi.

Akitangaza matokeo hayo, naibu meya wa Manispaa ya Iringa, Joseph Lyata alisema: “Kuanzia leo Kimbe si meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mpaka utaratibu mwingine utakapotangazwa.”

Wakati Lyata akieleza hayo, Njovu alisema kwa mujibu wa kanuni iwapo mchakato umekosewa sehemu yoyote, Kimbe anayo nafasi ya siku 30 ya kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana.

“Tafsiri ya kura halali inaeleweka, kura zilizoharibika tumeziona. Kama baraza tuliobaki tuendelee kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,” alisema.

Akisoma ripoti ya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya Kimbe katika mkutano huo jana, mwanasheria wa manispaa hiyo, Nicholus Nyakasungura alisema utaratibu uliotumika kufanya uchunguzi ni pamoja na kuona kama amekuwa akitumia vibaya madaraka.

“Kamati imeshauri kuzingatia sheria na taratibu za kanuni za kimaadili na ilipendekeza kuendelea na mchakato wa kumuondoa madarakani na kuitaka Takukuru kuchunguza mali za Kimbe jinsi alivyozipata,” alisema.

Alichokisema Kimbe

Lakini Kimbe alisema: “Mimi bado naitwa meya wa Manispaa ya Iringa. Kanuni yetu iko wazi inataka theluthi mbili ya wajumbe wote ndio wana uwezo wa kumuondoa Meya na mimi kura ambazo zimeharibika ni 12 kura halali 14 ndio zimepigwa, kwa hiyo wamekosa kura tatu ili waweze kunitoa.

“Ninajipanga kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana kwa sababu mchakato wa kuniondoa haujafuata taratibu na kanuni za kisheria.”

Naibu meya aeleza tofauti ya kura

Kuhusu hoja ya Kimbe kwamba mchakato haujazingatia taratibu, Lyata alisema kikao kilichoahirishwa (cha Machi 26) ndio kilihitaji akidi ya theluthi mbili.

“Leo (jana) kikao hakikuhitaji akidi hiyo. Kilichokuwa kinahitajika ni wajumbe waliopiga kura ndio inaangaliwa kwa sababu hata wote tusingefika wafike watatu bado wangeweza kumuondoa Meya na kama hajaridhika, akate rufaa kwa waziri husika,” alisema.

Madiwani Chadema walonga

Seveline Mtitu, ambaye ni diwani wa Mkimbizi, alisema tangu mchakato uanze tuhuma zilizotolewa dhidi ya Kimbe si za kweli.

“Majibu yaliyotolewa leo (jana) yalikuwa yamepangwa kwa misingi hiyo kama Kimbe atachunguzwa basi na mkurugenzi achunguzwe na Takukuru,” alisema.

“Cha msingi wangemuondoa katika hali ya utaratibu na kufuata kanuni. Wanapata faida gani kumuondoa Meya kwa miezi miwili iliyobaki?”

Lakini mbunge wa viti maalum (CCM), Ritha Kabati alisema alitegemea Chadema wangepiga kura ya hapana, lakini hawakufanya hivyo na matokeo yake kura zao zimeharibika.

“Kama walikuwa na haki yoyote walipaswa kuonyesha kwa maandishi kwamba hawajaafiki maelekezo ya tume ya uchunguzi, sasa kitendo cha kuharibu kura ni kumdidimiza mwenzao,” alisema.