MAKALA YA MALOTO: ACT ni wana demokrasia au wanafanya maigizo?

Thursday March 19 2020

 

By Luqman Maloto

Demokrasia ndani ya vyama vya siasa imekuwa sawa na maudhui kwenye mashairi ya nyimbo. Mwanamuziki anaimba mapenzi ya mfano wa kuigwa, lakini ya kwake yanamshinda. Analia mapenzi yasiyo na uaminifu, maisha ya kawaida yeye sio mwaminifu. Vyama vya siasa, hasa vile vinavyosaka fursa ya kuongoza dola, kilio chao kikubwa ni demokrasia. Kwamba vinakandamizwa na chama kinachoshika dola na kusababisha uwanja wa ufanyaji siasa usiwe tambarare.

Wakati huohuo, viongozi katika vyama hivyo vinavyowania dola, wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuhodhi madaraka, kurefusha muda wa kubaki ofisini na hata kucheza faulo nyingi wakati wa vipindi vya uchaguzi wa ndani ya vyama.

Ipo tabia inazoeleka sana, kwamba kiongozi wa juu kwenye chama ama anachaguliwa kwa kura za “ndio” na “hapana” au anasimama na mgombea dhaifu. Ni taswira hiyo imekuwa ikifanya wakosoaji wengi kulalamika kuwa vyama haviishi vinayo yahubiri. Vyama vinaingia kwenye migogoro mara nyingi kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa ndani au wakati wa uteuzi wa wagombea nafasi ya urais, wabunge na udiwani. Vyama vinalilia demokrasia, navyo vinaliliwa kukandamiza demokrasia.

Tuanze na mvutano uliokisamabaratisha chama cha NCCR-Mageuzi miaka ya 1990 kwa sababu ya makundi mawili, lile la aliyekuwa Mwenyekiti Augustino Mrema na la Katibu Mkuu, Mabere Marando. Mgogoro wa uongozi ulioibuka kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Mwenyekiti Chadema, uliosababisha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Chacha Wangwe, kusimamishwa uongozi mwaka 2008, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu. Chacha akasema alisimamishwa kwa sababu ya kuutaka uenyekiti uliokuwa na unaoendelea kushikiliwa na Freeman Mbowe. Mwaka 2009, mgogoro wa uenyekiti ukapamba moto Chadema, pale aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, alipotangaza kuchuana na Mbowe kuwania uenyekiti. Ilibidi wazee wa chama wamketishe Zitto atoe jina lake kwa kile kilichoelezwa angeendelea kugombea angesababisha mgawanyiko.

Mwaka 2014 ikawa zamu ya Zitto na maswahiba wake wa zamani, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kutuhumiwa kuandaa waraka wa kimapinduzi wenye maudhui ya kumuondoa madarakani Mbowe. Zitto, Kitila na Mwigamba walifukuzwa Chadema na kwenda kuanzisha ACT-Wazalendo. Mwaka 2019, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari alitangaza kujiweka pembeni na masuala ya siasa akidai chama hicho hakina demokrasia. Aliyekuwa Mwenyekiti Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye alitangaza kustaafu siasa, sababu ni ileile; uminywaji wa demokrasia ndani ya Chadema.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Vincent Mashinji naye baada ya uchaguzi wa Chadema, alijiunga na CCM.

Advertisement

Anzia Profesa Safari, Sumaye, Cecil Mwambe, Mashinji na wengineo ambao walihama wakati wa mchakato wa uchaguzi wa ndani na baadala yake, chukua sauti zao na kuzichuja kwenye spika utapata kitu kimoja; Demokrasia inaminywa.

Hicho ndicho kiliibua mgogoro CUF pia 2013 baada ya Hamad Rashid kuweka kusudio la kugombea ukatibu mkuu wa chama hicho dhidi ya Seif Sharif Hamad. Uamuzi huo wa Rashid ulisababisha mgogoro mkubwa, kisha alifukuzwa uanachama.

Hata kisa cha Safari kuondoka CUF na kukimbilia Chadema ni baada ya kuona hakutendewa haki alipogombea uenyekiti na kushindwa na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba. ACT - Wazalendo wamemaliza mchakato wa uchaguzi wao wa ndani. Viongozi wakuu wapya wamepatikana. Mambo mawili ambayo yanatosha kuwa alama ya demokrasia mosi, kila nafasi ilikuwa na wagombea. Pili, mazingira sawa ya kujinadi kwa wapigakura.

Kuna mambo hayakutarajiwa mfano Zitto kusimama dhidi ya mwanasiasa mashuhuri kwa siasa za Zanzibar, Ismail Jussa na Seif kuwania uenyekiti dhidi ya Shilungushela Kaheza na Yeremia Maganja. Kuna namna inaweza kusemwa kuwa hata aina ya ugombeaji ilikuwa magirini ili ionekane chama kina demokrasia ya wazi kwa wanachama wake, lakini lipo eneo ambalo huwezi kuwanyima sifa ACT; ni la mdahalo wa wagombea.

Seif na Shilungushela walikuwa na jukwaa sawa la kujinadi mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu, kama ilivyokuwa kwa Zitto na Jussa. Waliuza sera na hata kukosoana hiyo ni alama ya demokrasia ndani ya vyama ambayo ACT wameichora.

Advertisement