MAONI: Shughuli za maendeleo zisiathiri uhifadhi wa mazingira

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na mjadala mkubwa duniani kuhusu uhifadhi wa mazingira na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambayo kwa namna moja au nyingine inaharibu mazingira na viumbe vilivyomo ndani yake.

Wanaharakati wamekuwa wakionya juu ya athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na miradi ya maendeleo ambayo inasababisha mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, wanakubali kwamba siyo vibaya kufanya miradi ya maendeleo bali tahadhari za kimazingira hazina budi kuzingatiwa.

Suala la mabadiliko ya tabianchi na matokeo yake, ni miongoni mwa mambo ambayo yameuamsha ulimwengu kutafakari juu ya mustakabali wa maisha ya kesho, badala ya kufikiria mambo ya leo tu na kuangamiza vizazi vijavyo.

Kwa bahati mbaya, madhara ya uharibifu wa mazingira yanaonekana muda mfupi tu na binadamu wanaoishi sasa ndiyo wanaoumia na athari hizo kama vile hali ya jangwa, mafuriko, ongezeko la joto na kukosekana kwa chakula.

Mazingira na maendeleo ni mambo muhimu ambayo jamii zinatakiwa kuyakumbatia, lakini swali la kujiuliza ni namna gani tunaweza kuhifadhi mazingira wakati huohuo tukiendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo?

Jibu la swali hilo ni rahisi; tunaweza kufanya mambo yote mawili kwa ufanisi ikiwa tutaepuka vihatarishi vya uharibifu wa mazingira, kwa kuhakikisha kwamba ujenzi wa miradi ya maendeleo kama vile viwanda, barabara, reli au majumba hausababishi athari kubwa za kimazingira.

Hivi karibuni, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (Unep), Joyce Msuya, alisema Tanzania inaweza kujifunza juu ya maendeleo ya viwanda kutoka nchi za Korea Kusini na China.

Msuya alisema Korea Kusini na China zimeendelea baada ya kufanya uamuzi wa kujenga viwanda.

Hata hivyo, alisema nchi hizo zina mipango mizuri ya kuhifadhi mazingira katikati ya maendeleo ya viwanda waliyonayo.

Mwana mazingira huyo alimpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga viwanda hapa nchini na kueleza kwamba Afrika bado si mchafuzi mkubwa wa mazingira kwa hewa ya ukaa inayotoka viwandani, bali uchafuzi huo unatoka zaidi nchi za Magharibi.

Pia, alisisitiza kwamba zinahitajika juhudi za pamoja kupunguza uchafuzi huo ambao kwa bahati mbaya hauangalii mipaka ya nchi.

Tayari hatua kadhaa zimechukuliwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa lakini bado msukumo unahitajika zaidi.

Ninakubaliana na mtazamo wa Msuya kwa sababu ni vizuri kujifunza kwa waliopitia changamoto ambazo tunapitia sasa, ili tuweze kufanya uamuzi sahihi tukiwa na uelewa wa mambo na hatua stahiki za kukabiliana nayo.

Moja ya mambo ambayo Afrika inatakiwa kuyafikiria kwa sasa ni matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Mfano mzuri ni matumizi ya roboti katika kufanya kazi ili kupunguza uzalishaji wa takataka.

Ni kweli bara letu bado lipo nyuma kwa aina nyingi za teknolojia, lakini kwa hii ya matumizi ya roboti inawezekana. Ni teknolojia ambayo naamini haiwezi kuzishinda nchi nyingi za Kiafrika.

Kinachohitajika ni utashi tu wa watawala wa nchi katika bara hilo.

Pia, utoaji wa elimu kwa wananchi ni muhimu katika kupunguza madhara hayo.

Changamoto imekuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya uharibifu wa mazingira, kama vile matumizi ya mkaa ambayo yamekuwa makubwa kwa wakazi wa mijini.

Wananchi wakipewa elimu kuhusu athari za matumizi ya mkaa, watageukia mkaa mbadala na kuacha kukata miti kila siku kwa ajili ya kuchoma mkaa. Hilo linahitaji jitihada za pamoja za wadau na utashi wa kisiasa.

Vilevile, tulikuwa na matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini kwa muda mrefu, lakini Serikali imefanikiwa kupiga marufuku mifuko hiyo na sasa hakuna mifuko inayoonekana kwa wananchi. Huo ni utashi wa kisiasa ambao ulikosekana kwa muda mrefu. Na hili limethibitisha kuwa inawezekana kutekeleza yale tunayoyadhamiria.

Tunataka kuona utashi huo wa kisiasa ukiendelea kwenye mambo mengine ya kimazingira, ili kusukuma ajenda ya uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, ili tuifanye dunia hii kuwa sehemu salama ya kuishi.

Peter Elias ni mwandishi wa Mwananchi. 0763891422