MCL kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye mafuta, gesi

Muktasari:

Yaingia makubaliano na wadau wa mafuta na gesi ili kuchochea uchumi mkubwa  wa Taifa

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited(MCL) imesaini makubaliano ya kuandika maudhui yanayohusu uhamasishaji wa wananchi katika ushiriki wa fursa za sekta ya gesi na mafuta nchini.

Makubaliano hayo (MoU) yamefanyika kati ya MCL na Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi nchini(Atogs), ambayo imejikita kuhamasisha ushiriki wa wazawa kwenye sekta hiyo tangu miaka minne iliyopita.

Tukio hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam limehusisha pia makubaliano ya kampuni ya Rentco kutoka Kenya inayotoa mikopo na ukodishaji wa mitambo na vifaa mbalimbali kwa kampuni zenye mitaji midogo nchini.

Atogs pia imesaini makubaliano na Benki ya CRDB na Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) zitakazojikita na utoaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji kwa kampuni za ndani zitakazokuwa zikishiriki kwenye miradi mikubwa.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema;

"Kwa hiyo sisi kama Mwananchi Communication kupitia gazeti la The Citizen tunaangalia ni namna gani ambavyo tutatoa mchango katika ukuaji wa sekta ya mafuta na gesi kwa kutoa taarifa  zitakazowezesha watu kushiriki katika uchumi mkubwa.’’

“Kama mnavyojua gesi na mafuta ni uwekezaji mkubwa sana,ambao unahusisha kampuni kubwa kabisa za kimataifa na unahusisha teknolojia ya hali ya juu na inahusisha ujuzi wa hali ya juu.”

Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 na kanuni za ushirikishaji wa wazawa katika sekta ya gesi na mafuta ya 2017, zinaagiza kampuni za kimataifa kutumia kampuni za ndani kwa shughuli  za ununuzi wa bidhaa na huduma zitakazohitajika wakati wa miradi.

Hata hivyo,  Mkurugenzi wa Atogs, Abdulsamad Abdulrahim amesema kampuni za ndani zilizosajiliwa kwa ajili ya kutumia fursa hiyo zimekuwa zikikabiliwa na uwezo mdogo wa mitaji na vifaa kama mitambo ya uendeshaji wa miradi.

 

"Sasa wenzetu tumewaleta hapa ili kusaidiana wazawa washiriki katika miradi ya kimkakati,Rentco kazi yake ni kutoa bidhaa au chombo kwa Mtanzania anayetaka kushiriki katika miradi hii mikubwa, kama hana fedha anakuja kwa Rentco kukopa kwa kile kipindi ambacho anataka kutumia,"amesema Abdulrahim.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya TDB, Lloyd Muposhi amesema zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazowekezwa kwenye miradi hupelekwa nje kutokana na ushiriki mdogo wa kampuni za ndani

Utafiti wa mwaka 2016 chini ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC) ulibaini kampuni za ndani kwa wakati huo zingeweza kutumia wastani wa Sh1.4bilioni tu kati ya Sh17bilioni kwa hatua za awali za ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani katika mradi wa kiwanda cha kuchakata na kusindika gesi asilia(LNG) mkoani Lindi.