MIAKA 20 BILA NYERERE: Wanajeshi waasi jela miaka 10-6

Tuesday October 8 2019

 

Maasi hayo yalisababisha ghasia nyingi mitaani, hususan Mtaa wa Msimbazi maeneo ya Kariakoo. Maeneo mengi ya katikati ya mji risasi zilirindima. Mwarabu mmoja eneo la Magomeni, kwa kuona duka lake linavamiwa, alimpiga risasi mwanajeshi mmoja wa King African Rifles (KAR) aliyejulikana kwa jina la Kassim.

Koplo Nashon Mwita, ambaye alishuhudia mauaji hayo, alirudi kambini kujizatiti. Akiongozana na askari mwingine, Luteni Mwakipesile, pamoja na wanajeshi wengine wa KAR, walifika Magomeni na kummiminia risasi Mwarabu huyo.

Kama hiyo haikutosha, waliiteketeza nyumba yake kwa moto. Katika nyumba hiyo, inasemekana, Mwarabu huyo aliteketea na familia yake ya watu 15.

Maasi yalianza kusambaa haraka. Siku moja baadaye, Jumatatu ya Januari 20, yalifika hadi kambi ya jeshi ya Tabora ambako wanajeshi wengi wa KAR, kama Mrisho Kapteni Sarakikya, Luteni David Musuguri (mkuu wa zamani wa majeshi ya ulinzi JWTZ) na Luteni Abdallah Twalipo walikuwa wamepandishwa vyeo.

Jumanne ya Januari 21, maasi hayo yakafika Nachingwea—kambi ambayo ndiyo kwanza ilikuwa imeanzishwa, ikiongozwa na Meja Temple Morris.

Jumamosi ya Januari 25, 1964, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mwalimu Nyerere aliomba msaada kutoka Serikali ya Uingereza kunyamazisha maasi ya kijeshi yaliyokuwa yanazidi kusambaa katika Tanganyika. Hatimaye makomandoo wa Uingereza waliwasili kwa helikopta na kuwanyang’anya silaha waasi. Jioni ya siku hiyo hiyo maasi ya Tabora nayo yakazimwa.

Advertisement

Maasi hayo, hasa kambi ya Colito, yalizimwa baada ya makomandoo hao wa Uingereza kutua na kuanza kulipua lango la mbele la kambi hiyo. Mara moja askari walioasi walijisalimisha.

Kikosi cha Uingereza kiliongozwa na Brigedia Patrick Sholto Douglas. Waasi watatu waliuawa katika operesheni hiyo. 20 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa, kwa mujibu wa TIME (Jan. 31, 1964). Wengine walitoroka.

Kwa njia hiyo Rais Nyerere alirejea madarakani, lakini historia ya Tanganyika ikabadilika moja kwa moja.

Jioni ya Januari 25, baada ya kutembelea mitaa ya Dar es Salaam kujionea uharibifu uliofanywa na wanajeshi walioasi, Mwalimu alisikika moja kwa moja kupitia Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) akisema:

“Jana nililazimika kuomba msaada wa Mwingereza. Kwa bahati akakubali. Asubuhi hii kikosi cha kwanza kikawasili. Yote sasa ni shwari. Nasikia maneno ya wajinga kwamba eti Waingereza wamerudi Tanganyika.”

Zaidi ya hilo aliwachekesha waliokuwa wakimsikiliza. Alisema: “Askari wametuvua nguo. Tuko uchi. Jamaa wanasema tuazime nguo, nasema nguo ya kuazima bwana! ‘Unaweza kwenda kuazima ukapata baibui’.”

Wiki tatu baada ya maasi (Feb. 16, 1964), Mwalimu Nyerere aliitisha mkutano wa hadhara Viwanja vya Jangwani na kuwaambia Watanganyika hivi: “(Wanajeshi walioasi) Walidanganywa. Wendawazimu walikuwa wawili, watatu. Wale wengine waliswagwa tu. Wakivutishwa bangi, wakaja mjini kutenda maovu. Tukaenda kwa Mwingereza. Bwana Mwingereza tusaidie utuondolee balaa hili.”

Baada ya maasi hayo, Nyerere alianza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa hakuna kosa linalorudiwa. Hatua ya kwanza, kwa mujibu wa jarida TIME la Marekani (Feb. 07, 1964) alianza kukamata wote waliohusika.

TIME liliandika, “kupunguza uwezekano wa mfarakano wa mawazo, aliwabadilisha makamanda wa Kiingereza akaweka wa Kiafrika. Wakati huohuo, akateua kamati ya kutafakari mabadiliko ya kikatiba ambayo yataifanya Tanganyika kuwa nchi ya kidemokrasia ya chama kimoja kisheria na kiuhakika.”

Katika toleo lake la Januari 31, TIME liliandika, “Uso wake ulikuwa na simanzi. Hakuna hata Mtanganyika mmoja aliyeuawa kwa miaka yote 17 ya kupigania Uhuru wa Tanganyika. Lakini sasa baada ya uhuru Watangayika wameuawa.”

Jumanne ya Aprili 21, Mwalimu Nyerere alimwapisha Sir Ralph Wildham ndani ya Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika, na kumwambia awashughulikie kikamilifu wanajeshi waliofanya jaribio la kuipindua serikali yake hapo Januari 19, 1964. Ndipo Sir Wildham akatangaza rasmi kuwa wanajeshi wa kambi ya Colito waliotaka kuiangusha serikali watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, Aprili 27, 1964.

Wakati huo huo Rais alimteua Kapteni Abdallah Twalipo (35) na Kapteni Lukias Shaftaeli (39), wote wakiwa ni wanajeshi wa jeshi la Wananchi, kuwa wajumbe wa mahakama ya kijeshi. Sir Wildham akawa Rais wa mahakama hiyo. Baada ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mashitaka, Herbert Wiltshire Chitepo, alisema angewaita mashahidi 25.

Kesi hiyo iliendeshwa kwa siku chache na hatimaye hukumu ikatolewa. Ijumaa ya Mei 15, 1964, siku 19 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wanajeshi walioasi katika kambi ya Colito walihukumiwa, lakini adhabu zao zilikuwa tofauti.

Sajini Francis Hingo Ilogi alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela. Wengine wote walihukumiwa miaka 10 ambao ni Koplo Aliche, Koplo Baltazar, Private Jonas Chacha na Private Pius Francis.

Wengine waliohukumiwa miaka 10 ni Private Patric Said John, Sajini Lucas, Kapteni Kamaka Mashiambi, Kapteni Benito Manlenga, Private Dominicus Said. Waliohukumiwa miaka mitano ni Kapteni Andrea Dickson, Private Hamidus na Roger Mwanaloya.

Wanajeshi walioshitakiwa lakini hawakupatikana na hatia na hivyo kuachiwa huru ni Koplo Peter Mbasha, Private Ernao Msafiri, Private Gerado Raphael, Kapteni Mahara Magom na Kapteni Moses Kawanga.

Hata hivyo, hadi sasa maasi ya kijeshi ya mwaka 1964 ya KAR yamebaki kama fumbo lisilo na mfumbuaji. Yalikuwa ni mapinduzi ya kijeshi? Ulikuwa ni mgomo wa wafanyakazi? Mhusika mkuu alikuwa nani? Nani aliyeendesha nchi katika kipindi cha wiki ile iliyokuwa ngumu zaidi katika historia ya Tanganyika/Tanzania?

Rais alikuwa wapi kwa kipindi chote cha karibu juma nzima? Nani hasa aliyeita Waingereza au labda kumshauri Rais Nyerere kuita wanajeshi wa kigeni kuja kuzima maasi?

Je, wanajeshi hao walikuwa wakiasi dhidi ya maofisa wa kijeshi wa Uingereza tu? Pengine maswali haya na mengine mengi yanahitaji majibu ili kuitazama upya historia hiyo.

Itaendelea kesho...

Advertisement