MIAKA 20 BILA NYERERE: Nyerere ashtakiwa kwa kosa la uchochezi-3

Muktasari:

  • Oktoba 14 mwaka huu, Tanzania itatimiza miaka 20 bila Mwalimu Julius Nyerere. Alikuwa waziri mkuu wa kwanza Tanganyika na baadaye Rais wa kwanza Tanganyika na Tanzania. Makala haya yanaangazia maisha yake ya awali, elimu na harakati za kisiasa.

Mwaka 1958 Mwalimu Nyerere alishtakiwa kwa kosa la uchochezi kutokana na makala aliyoandika kwenye gazeti la chama cha Tanu lililoitwa ‘Sauti ya Tanu’. Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Pauni 150 za Uingereza (shilingi 3,000 za Tanzania wakati huo).

Tangu kilipoanzishwa Jumapili ya Julai 7, 1954, chama cha Tanu na rais wake Julius Nyerere, kilianza kuonekana kuwa mwiba mchungu kwa Serikali ya kikoloni. Kama ilivyo kwa harakati zote za kisiasa, Nyerere na Tanu walikabiliana na serikali ya kikoloni chini ya Gavana Edward Francis Twining.

Tanu walikuwa makini kuonyesha makosa yaliyokuwa yakitendwa na Serikali ya kikoloni, jambo lililowakera sana watawala wa kikoloni.

Kwa mujibu wa kitabu ‘A Gust of Plumes: A Biography of Lord Twining of Godalming and Tanganyika’ © 1972, mwaka 1957 Serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara iliyoendeshwa na Tanu kwa sababu matamshi yake yalichukuliwa kuwa ya chuki kwa serikali.

Lakini kwa kuhofia Umoja wa Mataifa, marufuku hiyo iliondolewa baadaye mwaka huo ingawa Serikali hiyo iliendelea kuwawekea Tanu vikwazo vya kisiasa.

Baada ya Nyerere kukerwa na unyanyasaji wa kisiasa wa Serikali ya wakoloni, Jumanne ya Mei 27, 1958 aliamua kuandika makala katika gazeti la ‘Sauti ya Tanu’ akiwashutumu wakuu wa wilaya wawili kwa kuwaita ni “washenzi na maharamia.”

Ingawa kuna marejeo fulani yanadai kuwa makala hiyo alichapisha Mei 7, 1958, ambayo ilikuwa Jumatano, marejeo mengi yanakubaliana ilikuwa Mei 27 na toleo la gazeti lilikuwa ni namba 29.

Katika makala hayo, kinasema kitabu ‘The Making of Tanganyika’ Judith Listowel © 1965, Nyerere alidai kuwa wakuu hao wa wilaya walikuwa wakifunga matawi ya Tanu Geita na Mahenge na kula njama za kuwaadhibu machifu walioiunga mkono Tanu. Sehemu ya makala hayo inasema: “Jamaa hawa wanawaghilibu watu waape uwongo kortini ili kuisingizia Tanu. Hawa hawa wanawapotosha watu na kuwaadhibu wasiokuwa na hatia. Jamaa hawa wanajidai kuhifadhi sheria na utangamano...

“Hatuiogopi sheria, ikiwa polisi hawajiingizi katika mambo ya siasa na kuamuru kati ya watiifu na wengine pamoja na magavana wa msituni, wanaojidai sheria haiwahusu, hapo basi, sheria inatufaa sana. Sababu za hawa wendawazimu kuwachokoza watu wafanye matata ni kuwa hatushindwi tukiwa watii wa sheria. Njama zao zimewatatanisha wenyewe walipofunga ofisi ya Tanu.

“Ikiwa Tanu haina dosari wataingiza ulaghai, uchochezi na fitina ili watimize shabaha zao za kishetani. Naiomba Serikali ya kibeberu itamke wazi kuwa inaishambulia Tanu kwa sababu tumetangaza wazi bila woga kuwa serikali ya mabavu tutaipiga vita. Tutaishambulia bila kupumua mpaka tumeiangusha. Hatutashika silaha, hatutatumia udanganyifu. Tutazitumia njia hizi kama vile tunavyotangaza nia yetu. Hatutavumilia kuonewa.”

Baada ya kuchapishwa makala hayo, Nyerere alikamatwa, akashtakiwa. Hiyo ni kwa mujibu wa mwandishi Kiluba Nkulu katika kitabu chake, ‘Serving the Common Good: A Postcolonial African Perspective on Higher Education.’

Katika kitabu cha ‘kesi ya Julius Kambarage Nyerere,’ mwandishi Simon Ngh’waya anaandika “baada ya wiki moja kupita, Serikali iliamua kuanzisha kesi ya kashfa dhidi ya Nyerere... Tarehe 5 Juni, 1958 saa 10:30 jioni, makao makuu madogo ya sasa ya chama, barabara ya Lumumba, Dar es Salaam, ... yalivamiwa na askari polisi wa Idara ya Upelelezi wakiongozwa na kaimu kamishna wa polisi aliyejulikana kwa jina la M. T. Mackinley.”

Nyerere alifikishwa mahakamani Jumatatu ya Juni 9, 1958 akikabiliwa na mashtaka matatu ya kashfa katika kesi namba 2207/58. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Jumatano ya Julai 9, 1958.

Hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo ni L.A. Davies. Mwanasheria wa Serikali na kiongozi wa mashtaka alikuwa J.vC. Summerfield. Wanasheria waliomtetea Nyerere ni Mahamoud Rattansey na Kantilal L. Jhaveri. Nyerere alisimama kizimbani kwa makosa ya kuwakashifu DC Weeks wa Musoma na DC Scott wa Songea.

Alipoanza kutoa ushahidi Agosti 11, 1958, Nyerere alikiri ndiye aliyechapisha makala hayo na aliyeandika akiwa na shabaha ya kuitaka Serikali itupie macho malalamiko ya watu.

“Sikutaka kuyaandika malalamiko hayo mapema hadi nilipogutushwa na kitendo cha Serikali kuyafunga matawi ya Tanu Geita,” alisema Nyerere.

Mahakama ilipokutana tena Jumatano ya Julai 16, 1958 upande wa mashtaka uliamua kufuta shtaka la kwanza dhidi ya mshtakiwa Nyerere. Kadhalika upande wa mashtaka uliamua kulifanyia marekebisho shtaka la pili lililokuwa linamkabili. Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Jumatano ya Agosti 13, 1958. Nyerere alitiwa hatiani. Sehemu ya hukumu ya Hakimu Davies inasema “Nyerere hakuwa na haki kisheria, kwa njia yoyote ile, wala kuwajibika kijamii alipoamua kuandika maneno hayo ya kashfa hadharani! Haukutolewa ushahidi wowote mbele yangu kuthibitisha kwamba Nyerere alichukua jukumu lolote kupeleleza madai dhidi ya Scott. Nyerere alikiri katika ushahidi wake kwamba alifahamu kuwa Scott hakufunga tawi la Tanu. Lakini alikuwa akitekeleza sheria alipokataa kuliandikisha tawi hilo la Tanu. Kwa hiyo, Nyerere hakufanya hivyo kwa nia njema.

“Isipokuwa aliandika maneno hayo ya kashfa kwa sababu anazozifahamu mwenyewe, siwezi kuridhika na maneno yake kwamba maneno aliyoyaandika yalikuwa ya kweli, hasa ikizingatiwa kwamba hakuwa na upendeleo wa aina yoyote kuandika maneno hayo.” Hakimu alimaliza kusoma hukumu yake na akasema Nyerere ana hatia kama alivyoshitakiwa. Baada ya maoni ya kisheria na ilipoonekana hilo ni kosa la kwanza la Nyerere, Hakimu Davis akatoa adhabu. Akasema “namtoza mshtakiwa faini ya Sh3,000 au jela miezi sita. Nampa mshtakiwa siku mbili kulipa faini hiyo.” Nyerere alilipa faini na kuachiwa huru.

Ingawa Nyerere alipewa nafasi ya kulipa faini na hivyo kuachiwa huru, si wote walikuwa na bahati kama yeye kwenye kesi hizo za uchochezi zilizofunguliwa na Serikali ya kikoloni.

Mhariri jela kwa uchochezi

Yote hayo yalianza mwaka 1955 wakati Baraza la Kutunga Sheria la kikoloni lilipopitisha sheria waliyoiita ‘Incitement to Violence Act’ ambayo kwa kukosoa tu watu wa rangi nyingine kungetosha kukufungulia mashtaka ya uchochezi na mzigo wa kuthibitisha kuwa hukutenda kosa hilo.

Mhariri wa gazeti la ‘Mwafrika’ hakupata bahati aliyoipata Nyerere. Gazeti hilo lililokuwa linatoka mara mbili kwa juma, lilikuwa linahaririwa na Robert Moses Makange, ambaye awali alikuwa katibu mkuu msaidizi wa Tanu na mjumbe wa kamati kuu ya Tanu, lilitolewa mara ya kwanza mwaka 1957 kama gazeti la kwanza la kisiasa lililochapishwa na Waafrika.

Makange alikuwa mwandishi na mhariri tangu lilipoanzishwa mwaka 1957 hadi 1961. Ukiondoa muda aliotumikia kifungo gerezani. Gazeti hilo lilifanya kazi kubwa ya kueneza siasa ya Tanu ya kudai uhuru. Katika toleo namba 19 la Jumapili ya Juni Mosi, 1958, gazeti hili liliandika hivi:

“Sisi wote tunajua kuwa Mwingereza yupo hapa kwetu kwa sababu ya kutunyonya damu na kujipatia manufaa yake mwenyewe, na wala asitudanganye kwamba yupo hapa kwa kuwa anatuonea huruma na kutaka kutufundisha ustaarabu au kuleta maendeleo ya nchi. Maneno haya ni kigeugeu cha kutaka kutufunika macho; na kwa kadri atakavyozidi kuwa hapa ndivyo madini na fedha zitakavyozidi kutolewa katika nchi hii kupelekwa kwao, ambako bila ya sisi hawawezi kuishi sawasawa.”

Baada ya habari hiyo, Makange na mchapishaji wake, Kheri Rashidi Baghelleh walikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi. Kutokana na sheria ya kikoloni iliyotajwa hapo juu iliyotungwa miaka mitatu kabla, Makange na Baghelleh walishindwa kesi hiyo. Hata baada ya kukata rufaa walishindwa pia.

Hatimaye walifungwa miezi sita na Serikali ya mkoloni kwa tuhuma za uchochezi uliodaiwa kuwa ungeweza kusababisha vurugu za ubaguzi wa rangi.

Pamoja na kwamba walihukumiwa kwenda gerezani, gazeti hilo halikupigwa marufuku, pengine kwa hofu ya watawala kwamba hali ingekuwa mbaya zaidi. ‘Mwafrika’ likampata mhariri mpya, Joel Mgogo.

Walipotoka gerezani Desemba 1958 walipata mapokezi makubwa kutoka kwa vijana wa Tanu waliojipanga barabarani kuanzia gereza walilokuwa wamefungwa hadi yaliko makao makuu ya chama Mtaa wa Lumumba.

Mwaka uliofuata, 1959, chama cha Tanu kiliacha kulifadhili gazeti hilo na badala yake kikaanzisha gazeti mbadala lililoitwa ‘Ngurumo’ ambalo lilichapishwa mara ya kwanza Jumatano ya Aprili 15, 1959 kama gazeti la kila siku.