MKUTANO WA SADC: Serikali ya Tanzania yavipongeza vyombo vya habari

Muktasari:

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) ambapo Rais wa nchi hiyo, John Magufuli aliuongoza kwa nafasi yake ya Mwenyekiti na kumalizika jana Jumapili huku waziri mwenye dhamana ya habari akitoa pongezi kwa vyombo vya habari jinsi vilivyoripoti mkutano huo.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe amevipongeza vyombo vya habari nchini humo kwa kazi kubwa ya kiuzalendo na weledi wa hali ya juu waliouonyesha katika kutangaza Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).

Shughuli za mkutano huo mkuu uliofanyika kuanzia juzi Jumamosi Agosti 17,2019 na kumalizika jana Jumapili zilianza Agosti 5,2019 kwa wiki ya biashara ya viwanda na mikutano mbalimbali iliyohusu jumuiya hiyo.

Dk Mwakyembe alitoa pongezi hizo jana Jumapili mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo ambao Rais wa Tanzania John Magufuli alikuwa akiuongoza kwa nafasi yake ya Mwenyekiti mpya wa Sadc inayojumuisha nchi 16 wanachama.

Alisema uandishi wa habari wa kujenga na kukosoa ambao una lengo la kurekebisha unahitaji kupongezwa kwakua unasaidia jamii na Serikali katika kuleta maendeleo ya haraka kwa Taifa.

“Waandishi wa habari mbali na kuutangaza Mkutano wa 39 wa SADC lakini pia wametumia taaluma yao kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini kupitia sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika viwanda, utalii, uchukuzi na nyinginezo,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza uwenyekiti wa Tanzania ambao unaendeshwa na Rais Magufuli umeleta ari na matumaini mapya ambayo yatasaidia nchi wanachama kuondoa vikwazo vingi vya kibiashara na mawasiliano ya karibu baina ya nchi wanachama  na kujenga ustawi wa uchumi kwa nchi hizo.

Waziri huyo alisema baada ya lugha adhimu ya Kiswahili kutangazwa rasmi kuwa miongoni mwa lugha nne zinazotumika ndani ya jumuiya hiyo, amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa za lugha hiyo ikiwemo uandishi wa vitabu vya kiada, ufundishaji wa lugha hiyo, kuuza sanaa zinazotokana na lugha hiyo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.