MRADI WA MACHINJIO: Agizo la JPM Vingunguti lapita muda

Dar es Salaam. Maelekezo ya Rais John Magufuli ya kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti yameshindwa kutekelezeka kwa wakati.

Ujenzi huo ulio chini ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na mshauri mwelekezi M/Scons Africa Limited na FB Consultant ulipaswa kukamilika Desemba 31, mwaka jana lakini Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri alisema haujakamilika kutokana na mvua.

“Kasi ya ujenzi wa machinjio ilikuwa ni kubwa na ilitendeka usiku na mchana, isipokuwa mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha mfululizo zilisababisha ujenzi kusimama mara kwa mara,” aliliambia Mwananchi alipopigiwa simu jana.

Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza, Septemba 16, mwaka jana katika machinjio hayo, akaeleza kutoridhishwa na mazingira ya eneo hilo na kasi ya ujenzi wa machinjio ya kisasa.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa Juni 2019, ulipaswa kukamilika baada ya miezi 18, lakini Rais Magufuli alifupisha mpaka miezi mitatu.

“Haiwezekani jengo la ghorofa moja tu lijengwe kwa miezi 18. Natoa maelekezo kuwa ndani ya miezi mitatu yaani Oktoba hadi Desemba 31 mwaka huu, ujenzi uwe umekamilika,” Rais alisema alipotembelea mradi huo.

Mapema Novemba, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia alitembelea mradi huo unaogharimu Sh12.5 bilioni.

Majaliwa pia alisisitiza machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini yakamilike mwishoni mwa Desemba 31, 2019 kama alivyoamriwa na Rais.

“Nimeambiwa kuwa ujenzi umekamilika kwa asilimia 60 mpaka sasa. Nataka ndani ya siku 28 zilizobaki, ujenzi wa mradi huu uwe umekamilika,” alinukukuliwa Majaliwa baada ya ziara yake.

Hata hivyo, Mwananchi ilitembelea eneo la ujenzi, Januari 1, mwaka huu, ambapo lilishuhudia kuwa mradi wa machinjio hayo mapya ukiwa bado haujakamilika.

Ujenzi wa jengo ulikuwa umefikia hatua ya kupaua, huku wafanyakazi wakiendelea na shughuli za kujaza vifusi, kupiga lipu na kupaka rangi baadhi ya maeneo.

Shauri alieleza kuwa kwa sasa wataalamu wanafanya tathmini ya kujua kiasi cha ujenzi kilichobakia kitachukua muda gani kukamilika.

“Baada ya mvua kubwa za mfululizo, tumeamua kufanya tathmini ya kiasi gani kimebaki cha ujenzi na muda gani utatosha kumalizia. Tathmini ikikamilika tutaujulisha umma,” aliliambia Mwananchi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wafanyabiashara ya Mifugo na mazao yake wa Vingunguti (Uamivi), Joel Meshaki aliliambia Mwanachi kuwa mpaka sasa hakuna soko maalumu la kuuzia nyama.

“Mpaka sasa nyama zetu tunauzia hapahapa machinjioni. Wanunuzi wa jumla hupaki vyombo vya usafiri nje na kuingia kununua kitoweo kwenye machinjio,” alisema.

Meshaki alisema zoezi hilo linahatarisha usalama wa nyama kutokana na ukweli kwamba eneo la kuchinjia kuna uchafu mwingi ikiwemo damu, kinyesi na takataka nyingine za binadamu.

Hata hivyo, Shauri alijibu kuwa ofisi yake bado inatafuta eneo maalumu karibu na machinjio kwa ajili ya soko la jumla la nyama.

“Kwa sasa tunaangalia namna ya kuhamisha baadhi ya wakazi kwa kuwalipa fidia ili watuachie eneo kwa ajili ya nyama,” alisema.

Kukamilika kwa machinjio hayo, kutaifanya nyama inayochinjwa ikubalike kwenye masoko ya nje ya nchi, hatua ambayo itaongeza mzunguko wa fedha kwenye eneo hilo wakati Serikali na Manispaa watanufaika kwani kutakuwa na ongezeko la makusanyo ya kodi.

Kwa sasa Manispaa ya Ilala hukusanya zaidi ya Sh118 milioni kwa mwezi wakati Serikali Kuu inapata Sh117 milioni kila mwezi.

Kwa mujibu wa meneja wa mradi huo wa machinjio, Mburuga Matamwe ameeleza idadi ya mifugo inayochinjwa katika machinjio hayo itaongezeka mpaka kufikia ng’ombe 1,000 kutoka 500 wa sasa na mbuzi na kondoo 500 kutoka 250.

“Mradi huu ukikamilika, mifugo yote itachinjwa kwa mitambo ambayo itasimikwa katika machinjio,” alisema.

Mitambo hiyo inahusisha ile ya kuchinjia, mikasi ya umeme ya kukatia kwato na pembe, mashine za kuchuna ngozi na mikanda ya kusafirishia nyama na bidhaa za nyama kutoka sehemu moja na nyingine.

Pia jengo hilo litakuwa na sehemu ya kuchinjia, kuvujishia damu, matanki ya kuhifadhia damu na maji taka na sehemu ya kuhifadhi kwato na pembe.

“Kutakuwa na vyumba nane vya kuhifadhia nyama (cold-rooms) vyenye uwezo wa kuhifadhi ng’ombe 580 waliochinjwa na mbuzi na kondoo 160 waliochinjwa kwa wakati mmoja,” alisema Matamwe.

Pia kutakuwa na maduka maalumu ya kuuzia nyama, vyakula na jenereta la ziada kwa ajili ya kufua umeme endapo umeme wa gridi ya taifa (Tanesco) utakatika.