MSHIKAMANO: Wanataka kuiweka Tanzania njiapanda

Dar es Salaam. Wanataka kuliwekaTaifa njiapanda, watu wanaombeana mabaya, wanafurahia mabaya ya wenzao. Ndiyo hali ilivyo nchini kwa sasa ikiashiria dalili mbaya.

Imekuwa kawaida hivi sasa kuibuka makundi mawili iwapo kwa kiongozi-- awe wa upinzani, chama tawala au serikalini-- anapatwa na mabaya; wako wanaomuombea mabaya zaidi na wako watakaoonyesha kuumizwa.

Si kwa binadamu pekee, hata vitu. Ndege za Shirika la Tanzania (ATCL) zikiharibika, huwa ni habari njema kwa kundi moja na habari mbaya kwa jingine.

Au mfano ni ile iliyoshikiliwa nchini Canada wapo waliofurahia na wapo walitetea kwa hali na mali.

Hata wakati ilipozuiwa Afrika Kusini kwa amri ya mahakama, wapo walioshangilia na walioumia moyo.

Matukio mengine yaliyogawanya watu ni kama shambulizi la risasi dhidi ya Tundu Lissu ambaye alikuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), ajali aliyopata Dk Hamis Kigwangalla (waziri wa maliasili na utalii) au Dk Mwigulu Nchemba (mbunge wa Iramba Magharibi-).

Hisia tofauti ziliibuka juu ya matukio hayo, baada ya baadhi kudiriki kusema bora wangefariki dunia na wengine kuungana nao katika machungu na hata kuwaombea na kuwatia moyo kwa kadhia hiyo.

Tukio jipya ni la wiki iliyopita wakati ulipozuka uzushi mitandaoni kuhusu afya ya Rais John Magufuli. Baadhi walitoa maneno yaliyoonyesha hawamtakii mema na wengine wakimwombea kheri na hata kusema “Mungu atuepushie mbali”.

Hali hii inazidi kukua miongoni mw jamii kiasi cha kutishia mwelekeo sahihi wa nchi ambayo imejijengea amani, utulivu na mshikamano kwa miaka yote ya uhuru wake.

Mshikamano huo, amani na utulivu sasa unatishiwa na chuki inayojengeka taratibu miongoni mwa jamii, huku matumizi ya mitandao ya kijamii yakiweka bayana hali ya mgawanyiko katika Taifa ambao umeanzia kwa chuki dhidi ya viongozi.

“Kama una chuki dhidi ya kiongozi au mtu fulani, mfuate umweleze ili msameheane badala ya kuombeana mabaya,” alisema ofisa habari wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kayomo alipotoa maoni yake kwa Mwananchi kuhusu chuki zinazojipambanua katika mitandao ya kijamii.

“Kuna kitu kinaitwa ibilisi ambaye ni adui anayeweza kumuingia mtu yeyote na kumfanya amchukie mtu kwa jambo fulani.

“Si jambo la busara kumuombea mabaya binadamu mwenzako. Lazima Watanzania waishi kwa upendo, amani na mshikamano.”

Maoni kama hayo yalitolewa na sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum.

“Mungu hapendi kumcheka mtu akiwa anaumwa, mlemavu au amefariki dunia kwa sababu vitu hivyo vinaweza kukurudia mwenyewe,” alisema Alhaj Salum.

“Watu wanaochekelea wenzao wapate mabaya, wamekosa imani miongoni mwao.”

Alisema dini zinafundisha na kuelekeza kuwaombea viongozi wa kitaifa ili wawe na afya njema na akili timamu na hivyo watekeleze majukumu yao kwa ufanisi kwa sababu ni watu muhimu kwenye jamii.

“Ni jambo la kukemea hili. Hawa ni watumwa, si waungwana. Muungwana hawezi kumuombea mabaya mwenzake. Kinachotakiwa ni watu kumrudia Mungu na mafundisho ya imani za dini zao.”

Sheikh huyo alisema kinachosababisha masuala hayo kujitokeza ni chuki zinazostahili na zisizostahili kwa baadhi ya watu dhidi ya watu fulani ambao wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mtazamo wa Sheikh Alhad unafanana na wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge –Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemuguzi aliyesema Mungu amemuumba binadamu akitaka watakiane mema hata pale wanapotendewa mabaya.

“Mtu anayemtakia mwenzake mabaya, namtoa kwenye kundi la wema na kumuweka kwenye kundi la watu wabaya,” alisema Askofu Niwemuguzi.

“Kila mmoja arudi kwenye nafsi yake na atambue ameumbwa kwa mfano wa Mungu ambaye anatutakia heri na sisi tuwatakie wenzetu,” alisema Askofu Niwemugizi.

Wanasiasa: Chuki za kisiasa

Lakini wanasiasa wanaona hali hiyo imetokana na chuki za kisiasa ambazo zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema ni rahisi mtu mmoja kumuombea mabaya mwenzake akidhani atafanikiwa.

“Tumeshindwa kusimamia utawala bora miaka ya themanini pamoja,” alisema

Dk Mashinji alisema kinachotakiwa ni watu kumrudia Mungu na kuhimiza utawala wa sheria uchukue nafasi ili kurudisha utamaduni wa kutakiana pole na kheri.

Mtazamo huo unaungwa mkono na kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

“Hii ni dalili kwamba jamii yetu ina mpasuko, kamba au uzi unayoisuka jamii nzima ambayo ni utu, umoja na upendo imekatika na ndio maana watu wanashangilia mabaya yanapowapata wengine,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

“Hili jambo limeshika kasi sana katika utawala wa awamu ya tano, tofauti na utawala uliopita. Umepanda madaraja na chuki na umejenga utamaduni kwamba ili uweze kuthaminiwa lazima ujipendekeze.”

Kipi kifanyike. Zitto anasema “turudi katika siasa zilivyokuwa kabla ya mwaka 2015. Tukisharudi hapo, Watanzania wanarudi pamoja, ikitokea madhila wanarudi pamoja, ikitokea nini Rais anakutana na wapinzani wanazungumza na kuyamaliza. Hili ni jambo hatari na halina afya kwa taifa.”

Hatari hiyo pia anaiona naibu katibu mkuu wa CUF- Bara, Magdalena Sakaya, ambaye anashauri kuwepo mjadala.

“Si jambo zuri. Kama Taifa tukae pamoja tuhitimishe mjadala utakaowezesha kuwa na amani na furaha kwa Watanzania wote,” alisema Sakaya.

Hata hivyo, katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga hakutaka kuzungumzia suala hilo alipoulizwa maoni yake kuhusu chuki zinazoonekana kuenea miongoni mwa jamii, hasa kwa wanaotumia mitandao ya kijamii na mustakabali wa Taifa.

Si utamaduni wa Mtanzania

Wakati wanasiasa wakiona jambo hilo linatokana na masuala ya kisiasa, mwanasheria wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke anaona utamaduni mpya ukijengeka katika jamii.

“Huu si utamaduni wa Mtanzania kwa sababu Taifa limejengwa kuishi kwa umoja na mshikamano. Wanaofanya hivyo hawako sahihi,” alisema.

“Wanaombea mabaya au kusema maneno hayo wana chuki na hawako sahihi. Hawathamini utu na hulka za Mtanzania, hizi ni kebehi inabidi zipuuzwe.

“Tumelelewa kwa misingi ya utamaduni wa kushirikiana na umoja na wanaofanya hivyo vitendo wamekosa maadili. Utamaduni wetu ni kuishi kwa pamoja na kushirikiana.”

Naye Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema hali hiyo inatokana na siasa kujengwa kwenye hali ya chuki tofauti na awali wakati viongozi walipokuwa wakishirikiana, kusalimiana na kutakiana heri kwa kila jambo.

“Miaka iliyopita watu hawakuwa wakiombeana mabaya. Kulikuwa na siasa za ushindani kuliko hivi sasa. Turudi kwenye siasa za undugu umoja na mshikamano kwa sababu wote ni kitu kimoja,” alisema Ole Ngurumwa.