Maalim Seif afunguka kuhusu adhabu yake

Saturday October 17 2020
maalimpic

Mgombea Uraisi wa Zanzibar kwa chama cha ACT- Wazalendo Malim sefu sharifu Hamad akizungumza na waandishi wa habar Unguja Zanzibar jana.Pich na mpiga picha maalum

Unguja. Siku moja baada ya Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kumfungia kwa siku tano kutofanya kampeni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatakata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Maalim Seif ambaye alisema hatafanya hivyo kwa sababu hana imani na ZEC na haitamtendea haki kwenye mchakato huo.

Juzi Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilimtiani hatiani Maalim Seif na kkumfungia kufanya kampeni siku tano baada ya kudaiwa kwenda kinyume na maadili ya uchaguzi.

Katibu wa kamati hiyo, Khamis Issa Khamis alieleza juzi kuwa hatua ya kumfungia Maalim Seif imekuja kufuatia malalamiko ya mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir kwamba Maalim Seif alikiuka maadili akiwa Pemba kwenye kampeni zake Oktoba 13 zilizofanyika Jadida Wete.

Alisema katika malalamiko hayo Maalim Seif alidaiwa kuwataarifu wanachama wake kwamba wajitokeze kwa ajili ya kupiga kura tarehe 27 kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha cha 82 (1) (2) cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kinawataja watu maalumu wakiwamo watendaji wa uchaguzi kwamba ndiyo watakaohusika kupiga kura siku hiyo ya uchaguzi mkuu.

Akizungumza na gazeti hili jana mgombea huyo alisema “kwanza sitokataa rufaa, pili ni jambo nililolitarajia, hivyo sikushtuka hata kidogo. Naamini CCM ina hofu ya mkutano wangu wa Nungwi.

Advertisement

“Hivyo ndiyo njia yao ya kunizuia, haitawasaidia chochote kwa sababu Wazanzibari wameshaamua CCM ikae pembeni,” alisema mgombea huyo.

Alipoulizwa iwapo atapumzika au ataendelea na shughuli za chama? Maalim alisema “chama kitaamua kuwa nipumzike au nifanye shughuli nyingine za kuimarisha chama. Pia chama kitafanya marekebisho ya ratiba kuanzia tarehe 21.”

Kwa mujibu wa ratiba za mikutano ya kampeni za Maalim Seif, jana Ijumaa alikuwa kwenye mapumziko, leo alitakiwa awe jimbo la Mtoni na kesho Nungwi ambako angefanya mkutano wa hadhara.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, anaingia kwenye orodha ya kina Tundu Lissu, Halima Mdee, Gervas Mgonja na Maftaha Nachuma ambao waliwahi kufungiwa kampeni zao kwa siku tofauti upande wa Tanzania bara.

Katika mkutano wake wa juzi uliofanyika Uwanja wa Muwanda –Donge akiomba kura na kujinadi Maalim Seif alisema endapo akifanikiwa kuingia madarakani Oktoba 28 atahakikisha kila Mzanzibari anakuwa na uhakika wa mlo kamili wa mwezi mzima.

“Hutoomba chakula kwa mtu, pia kila mmoja atakuwa na nyumba bora anayostahili kuishi binadamu. Kila mmoja atakuwa na uhakika wa kuvaa mavazi anayotaka mwenyewe,” alisema Maalim Seif.

Advertisement