Maalim Seif ahofia kukosa uchaguzi mkuu Zanzibar 2020

Tuesday December 3 2019

 

By Tumaini Msowoya na Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hofu imetanda kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 baada ya ACT-Wazalendo upande wa Zanzibar kudai kuna njama za kuihujumu.

Miongoni mwa tuhuma hizo ambazo zimeelekezwa kwa CCM ni kuwapo kwa mpango wa kuiagiza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa muswada wa marekebisho ya sheria ya uchaguzi utakaowabana wagombea ambao hawajakaa katika vyama vyao vya siasa kwa angalau miaka mitatu.

Mshauri huyo mkuu wa ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad alidai mjini Unguja jana kuwa CCM iliandaa kikao kilichoazimia kuiagiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa muswada utakaoweka sharti la muda wa miaka mitatu wa uanachama ili kupata sifa ya kuwa mgombea wa nafasi mbalimbali.

Maalim Seif alidai muswada huo umepangwa kupelekwa kwa dharura kwenye mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaondelea sasa.

“Muswada ambao utaweka sharti la kwamba ili mtu aweze kugombea urais wa Zanzibar, uwakilishi, na udiwani basi ni lazima mtu huyo awe mwanachama wa chama cha siasa anachogombea kwa angalau miaka mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi,” alidai Maalim Seif.

Hata hivyo, CCM imejibu mapigo kuwa kauli hiyo ya ACT Wazalendo kwa kuita ni sawa na “wafa maji hawa maskini wanatapatapa.”

Advertisement

Maalim Seif alidai lengo la njama hizo ni kutaka kuwazuia wanachama wa ACT–Wazalendo waliojiunga na chama hicho kuanzia Machi mwaka huu, wasiweze kugombea uchaguzi mkuu ujao.

Kwa waliojiunga na ACT- Wazalendo Machi mwaka huu, mpaka wakati wa uchaguzi mkuu ujao watakuwa wamedumu kwa mwaka mmoja na nusu hivi ndani ya chama hicho.

“Kwa kufanya hivyo, CCM wanadhani wataweza kujiondolea upinzani mkali unaowakabili hapa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao,” alidai Seif, ambaye alijiunga na ACT-Wazalendo, Machi 19.

Hata hivyo, katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Catherine Peter alipozungumza na Mwananchi jana baada ya kupigiwa simu kujua kulikoni juu ya tuhuma hizo, alisema hazina ukweli wowote kwa sababu hakuna kikao kilichoketi kujadili ajenda hizo.

“Katibu mkuu yupo huku kweli, na amefanya vikao vya ndani na nje lakini hakuna mahali ajenda hizo zimejadiliwa, wafa maji hawa maskini wanatapatapa,” alisema Catherine.

Maalim Seif alidai pia wanazo taarifa za kuwapo njama za ofisi zao kuvamiwa na wafuasi wa CUF.

“Njama hizo ambazo zilipangwa zianze Jumapili iliyopita kisiwani Pemba na kisha ziendelezwe hapa Unguja... zimepangwa lakini kwa kuwatumia chama cha CUF ambao wamehakikishiwa kwamba watalindwa,” alidai Maalim Seif, ambaye chama chake pia kimetoa waraka kulalamikia kilichokiita njama za hujuma dhidi yao.

Maalim Seif alidai malengo ya mpango huo ni kutaka kuwakamata viongozi wa ACT–Wazalendo na kuwabambikia kesi.

Mwananchi lilimtafuta kiongozi wa CUF ili tuhuma hizo za katibu wao mkuu wa zamani.

Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa alikiri kuwa wanataka kufuata mali zao kwenye ofisi za ACT-Wazalendo.

“Analalamika nini Maalim Seif? Ni kweli tuna mpango huo wa kwenda kuchukua mali zetu, jana (juzi) tulifanya `road show’ Pemba (wafuasi walipita barabarani).

“Tulipata taarifa za kiintelijensia kutoka polisi kuwa ACT-Wazalendo wameandaa vijana kwa ajili ya kutufanyia vurugu pindi tutakapoenda kukomboa mali zetu walizozichukua kinguvu kinyume cha utaratibu na kujimilikisha,” alisema Khalifa.

Khalifa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Gando, Pemba, alisema wakati wowote watakwenda kuchukua mali zao mbalimbali zinazomilikiwa na ACT-Wazalendo zikiwemo ofisi na magari aliyodai yamehifadhiwa kwenye maghala yao.

“Zile ni mali za CUF siyo za kwao, ni aibu kwa mtu mzima kuiba mali zisizo za kwako. Maalim Seif tunamheshimu, aangalie tusije tukamvunjia heshima waziachie mali zetu,” alisema Khalifa wakati akizungumza na Mwananchi kwa simu.

Wakati wanachama wa CUF walipohamia ACT-Wazalendo wakiongozwa na Maalim Seif Machi mwaka huu walibadilisha majengo ya ofisi kadhaa kuwa za chama hicho kipya.

Maalim Seif alisema chama hicho kinadai kuwa maandalizi ya njama hizo yalianza mapema lakini yaliongezewa nguvu na ziara ya Dk Bashiru Ally baada ya kwenda Zanzibar.

Alilalamika kuwa katika ziara ya Dk Bashiru, vijana wa CCM walishusha bendera za chama chao kwenye kila mkoa uliokuwa na ziara ya kiongozi huyo.

Maalim Seif alisema, “tukio la kwanza la kushusha bendera ya ACT-Wazalendo lilifanywa siku ya Jumatano, Novemba 27, 2019 saa 6:00 mchana kwenye Ofisi ya Tawi la Bandamaji, Jimbo la Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.”

Alisema tukio jingine lilitokea Novemba 29 kwenye ofisi za Tawi la Mbuyuni, mkoa wa Kusini Unguja na kwamba matukio yote yameripotiwa polisi.

Alidai sababu za kufanyika njama hizo ni utafiti wa hali ya siasa na vyama kuelekea uchaguzi mkuu kuonyesha kuwa ACT – Wazalendo inaungwa mkono na watu wengi.

Wakati CUF ikikabiliwa na kibarua cha kulinda nguvu yake huko Zanzibar baada ya kuondoka kwa Maalim Seif, nayo ACT-Wazalendo kwa sasa inajipenyeza kwa kutumua turufu yao ya kiongozi huyo.

Nayo CCM kwa sasa ina nafasi ya kupenyeza nguvu zake kutokana na vita iliyopo baina ya CUF na ACT-Wazalendo ambazo zinanyang’anyana wanachama na matawi pia.

Advertisement