Breaking News

Maalim Seif aitwa Kamati ya Maadili

Friday October 16 2020

 

By Bakari Kiango

Unguja. Mgombea urais Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema amepokea barua ikimtaka afike katika afike mbele ya Kamati ya Maadili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kwa mujibu wa Maalim analalamikiwa na Chama cha Demokrasia Makini.

Maalim Seif alisema hayo jana kwenye mkutano wake wa kampeni alioufanya Magomeni mjini Unguja.

Alisema; “Nilikuwa nimepanga kuwahutubia wananchi wa Magomeni mjini Unguja kuhusu namna Serikali ya ACT Wazalendo inavyojipanga kupambana na rushwa inayoitafuna Zanzibar kimyakimya.

“Lakini nimepata barua kutoka ZEC eti nimeshtakiwa na chama kinachoitwa Demokrasia Makini, nyie mnakijua?” Hapanaaa” aliitikiwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

“Sasa hawa ndiyo wamenishtaki ZEC na nimeambia nifike kesho (leo) Saa 7 mchana mbele ya kamati ya maadili ya ZEC. Je,kosa lenyewe mnalijua? Wananchi wakajibu tena hapana. Nimeambiwa nimehatarisha amani ya nchi katika mkutano wangu wa juzi nilioufanya Jadida, Pemba kwa kusema wananchi wakapige kura Oktoba 27,” alidai Maalim Seif.

Advertisement

Akiwanadi wagombea wa viti vya uwakilishi, ubunge na udiwani akiwaombea kura.

Maalim Seif amerejea mjini Unguja jana akitokea Pemba alikokuwa akifanya kampeni kwa siku mbili.

Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Biman mgombea huyo amebakiza mkutano mmoja wa mwisho wa kufunga kampeni Pemba utakaofanyika Uwanja wa Tibirizi Oktoba 22.

Maalim Seif ambaye ni mwenyekiti wa ACT Wazalendo alisema “dhumuni la hiki chama kinataka nifungiwe kampeni kama ilivyokuwa kwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema, Tundu Lissu. Nitakwenda kuwasikiliza,” alisema.

Mgombea huyo, ambaye aliwahi kuwa Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 alidai viongozi hao wameamua kukimbilia Tume ya Uchaguzi ili wapate huruma, lakini kama wana hoja wangepanda majukwaani wakajibizana.

Awali Maalim Seif aligusia suala la rushwa akidai Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) imeshindwa kutimiza wajibu.

Alidai wapo mawaziri na vigogo visiwani humo wamejilimbikizia mali kinyume cha utaratibu, lakini hawafuatwi kuhojiwa na mamlaka hiyo au Tume ya maadili.

“Kuna mtu ana nyumba 37 hadi unajiuliza anakaaje kwenye nyumba hizo. Kuna baadhi ya mawaziri wana makasri zaidi ya matatu lakini hawaguswi,” alidai Maalim Seif.

Alisema Serikali ya ACT Wazalendo imedhamiria kupambana na hali hiyo mara tu ikiingia madaraka.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya ushindi wa kampeni za Maalim Seif , Mansoor Himid Yusuf aliwaondoa hofu Wazanzibari kuwaendapo mgombea huyo atashinda urais atawatumikia watu wote bila kujali itikadi zao.

“Atalinda haki zetu, atakuwa mtiifu kwetu na tutaishi kwa raha na furaha kwenye nchi yetu. Tumchague Maalim Seif ili kila mmoja wetu awe mwananchi wa daraja la kwanza ndani ya Zanzibar,” alisema Mansoor.

Advertisement