Maalim Seif awapigania wazee, wagonjwa dhidi ya corona

Muktasari:

Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesisitiza suala la wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya  maambukizi ya virusi vya corona (covid-19) vinavyoendelea kuitesa dunia.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad ameishauri jamii kuwalinda wazee na wagonjwa wa magonjwa mengine ili wasiambukizwe virusi vya corona (covid-19).

Amesema wazee wenye umri kuanzia miaka 70 na wagonjwa wenye maradhi mengine kama shinikizo la damu, moyo, kifua kikuu, kansa na kisukari ni rahisi zaidi kushambuliwa virusi hivyo kuliko wengine.

Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii leo Jumamosi,  Aprili 4, 2020, Maalim Seif amesema,“naomba sana wananchi muwalinde wazee wetu na wagonjwa kwa kutowakaribia sana kipindi hiki na waepusheni na misongamano ya watu.”

Amesema ikiwa mmoja kati ya walio kwenye kundi hilo ataonyesha dalili za kupanda homa au kukohoa ni vizuri afikishwe vituo vya afya ili apimwe na kusaidiwa haraka.

Maalim Seif amesema ni rahisi kuzuia maambukizi hayo ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wa kujilinda na kulinda wengine lakini vigumu kupambana na ugonjwa huo watu hawatakuwa makini.

“Iwapo kila Mzazibar atajitahidi kuhakikisha hakuna mgeni anayeingia nchini humu bila kwanza kupimwa tutazuia virusi kuingia nchini kwetu,” amesema Maalim Seif aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar

Maalim Seif amesema wataalamu wanasema virusi vya ugonjwa huo vinasambaa kwa kasi hivyo ni vizuri kwa jamii ikafuata maelekezo ikiwamo kutokaa kwenye mikusanyiko.

“Niwasihi sana wananchi ukiona dalili hizi epuka kukaa na watu, usipuuze ushauri wa wataalamu kukaa umbali walau wa mita mbili kutoka mtu na mtu, umbali huo unatisha kuzuia virusi kumfikia mwingine,” amesema Maalim Seif.

Amesema kushindwa kufuata miongozo ya afya ni kuwaweka wengine kwenye chanzo cha wengine kuteseka na ugonjwa huo.

Mpaka leo asubuhi Jumamosi, Tanzania ina jumla ya wagonjwa 20 wa corona kati yao watatu wamepona na moja amefariki dunia.