VIDEO: Maalim Seif awekwa mtu kati na CCM na CUF

Muktasari:

Mshauri mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amewekwa mtu kati baada ya jana kuelekezewa mashambulizi na vyama vya CCM na CUF.



Unguja/Dar es Salaam. Mshauri mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amewekwa mtu kati baada ya jana kuelekezewa mashambulizi na vyama vya CCM na CUF.

Maalim Seif alidai wiki hii kuwa CCM-- kwa kutumia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)-- wanapanga kukihujumu chama chake cha ACT-Wazalendo visiani Zanzibar kwa kushirikiana na CUF.

Maalim Seif alidai SMZ ina mpango wa kuwasilisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi kupendekeza moja ya sifa za mgombea uongozi wa Zanzibar awe angalau mwanachama wa chama cha siasa kwa miaka mitatu.

ACT-Wazalendo imeibuka kuwa tishio kwa vyama vya CCM na CUF kwenye siasa za Zanzibar baada ya Maalim Seif kujiunga na chama hicho Machi 19.

Maalim Seif na wanachama wengine waliondoka CUF baada Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa hukumu ya kukubaliana na uamuzi wa Msajili wa vyama vya siasa ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, Machi 18, mwaka huu.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti jana, katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na uongozi wa CUF walizungumzia madai hayo ya Maalim Seif.

Akizungumza jana wakati akihitimisha ziara yake kisiwani Pemba, Bashiru alisema hawezi kulumbana wala kumjibu Maalim Seif kwa kile alichokiita kutoona sababu ya kufanya hivyo.

Bashiru alishauri nafasi aliopewa Maalim Seif kwenye chama hicho angeitumia ipasavyo kushauri masuala yenye faida na ujenzi wa chama chake.

Dk Bashiru alisema mtu kama Maalim Seif anapaswa kujiepusha kuingia kwenye malumbano ambayo hayana tija kwa chama chake.

“Kwa miaka yangu kwenye siasa sijawahi kumuona Maalim Seif akizungumza kwa ukali namna ile, lakini mara hii amenishangaza,” alisema Bashiru.

Bashiru alidai huenda sababu ya ukali huo wa Maalim Seif umetokana na ziara yake kisiwani Zanzibar ambayo alidai imeleta tija kubwa sana ikiwemo kuongeza wanachama wapya hususani katika ngome yao ya upinzani kisiwani Pemba.

“Maalim Seif na wenzake wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kuwa muda unapotea,” alisema.

“Ni vizuri wakatumia muda wao kwa mambo muhimu ikiwemo ujenzi wa chama. Pia nawaomba wananchi wa Zanzibar kuacha kung’ang’ania kuunga mkono vyama vya upinnzani kwani ni kupoteza muda kwa sababu vimepoteza dira.

“Ni lazima mtumie akili zenu leo miaka mingapi mmewapa nafasi za uongozi wawakilishi na wabunge wa chama cha upinzani, wamewasaidia nini kuwaletea maendeleo?”

Katika hatua nyingine, uongozi wa CUF nao umemjibu Maalim Seif, ukikiri kuwa unaandaa operesheni ya kurejesha mali zao zilizochukuliwa na ACT-Wazalendo huko Zanzibar.

Mjumbe wa bodi ya wadhamini ya CUF, Musa Kombo aliwaambia waandishi habari jana kuwa chama hicho kimeanza ukaguzi wa ofisi zake zilizopo wilayani Chakechake, Pemba.

Kombo alisema wanachama wao wa CUF wakitumia misafara ya magari yapatayo 30 wamekuwa wakipita mitaani kutangaza operesheni hiyo.

“Zipo pia ofisi nyingi za majimbo na matawi zilizojengwa kwa michango ya wabunge na wawakilishi wote waliokuwepo tangu mwaka 2005 hadi 2015 ambazo zimevamiwa na kubadilishwa rangi.

“Chama kimoja cha siasa kinadai ofisi hizo sio za CUF bali tuliazimwa na waliokuwa wanachama wetu na sasa wanachama hao wamehamia chama hicho (ACT-Wazalendo) na kukabidhi ofisi hizo na kuzipaka rangi za chama walichojiunga nacho,” alieleza Kombo.

Kombo alitoa mfano kuvamiwa kwa ofisi ya CUF iliyoko jimbo la Micheweni kisiwani Pemba ambayo ilijengwa na aliyekuwa mbunge jimbo hilo, Shoka Khamis kupitia chama hicho.

Naye mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Nassor Amour amesema kwa mujibu wa ibara ya 10(3) ya katiba ya CUF inaeleza wazi kuwa hata kama mtu akitoa mchango au mali, anapofukuzwa au kuhama mali hizo zinabaki kuwa za chama cha CUF.

“Tunaenda kuchukua ofisi zetu na matawi yetu pamoja na zoezi la upandishaji wa bendera litakalofanywa na Mwenyekiti wetu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,” alisema Amour.

Pia Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Haroub Shamis amewataka wanachama wa chama hicho na wazanzibari kutotumiwa kumsikiliza mtu mmoja bila ya kumtaja bada yake kutumia katiba kuleta haki na furaha kwa wote.

“Tumechoka kugombanishwa na kupigana, ukiwa kiongozi unatakiwa kutumia nafasi hiyo kuleta maendeleo, imefikia mahali Zanzibar tufanye kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo,”alisema Shamis.

Katika madai yake, Maalim Seif, ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alisema anahofia muswada huo una lengo la kuwazuia yeye na wenzake waliohama CUF kufuatia mgogoro wa uongozi huko na kujiunga na ACT-Wazalendo, ambapo muswada huo ukipita watakosa sifa za kugombea.

Pia Maalim Seif alidai kuwa CCM ilikuwa inaitumia CUF kuwafanyia fujo kwa kuruhusu washushe bendera za ACT-Wazalendo na kuchukuliwa kwa majengo ya matawi yao huko Zanzibar.