Maalim Seif azungumzia kifo cha katibu mkuu CUF

Muktasari:

Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa alikitumikia chama hicho kwa uwezo wake wote.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa alikitumikia chama hicho kwa uwezo wake wote.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumanne Machi 31, 2020, Maalim Seif ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa CUF alimpa pole mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kubainisha kuwa chama hicho kimempoteza mtu muhimu.

“Pamoja na kasoro zake za kibinadamu alikuwa mzalendo aliyekipenda na kukitumikia chama  chenu cha CUF kwa moyo wa udhati.”

“Alijitahidi kutumia uwezo wake wote kukiimarisha chama chenu. Hapana shaka kifo chake kimewacha pengo kubwa,” amesema Maalim.

Ameongeza, “hatuna budi kurudi kwa Mungu.  Kila kiumbe kitaonja mauti,  mwenzetu siku yake imefika ni wajibu wetu kumshukuru Mungu na kumuombea marehemu Mungu amsamehe dhambi zake zote, amlaze pema peponi na wafiwa awape subira.”