ATHARI ZA MVUA: Mabaki ya viungo vya maiti vyazikwa upya Mwanza

Mwanza. Mabaki ya viungo vya binadamu yaliyopatikana baada ya mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini Mwanza mwishoni mwa wiki na kufukua makaburi imezikwa upya.

Mvua hiyo iliyonyesha kwa zaidi ya saa moja, ilisomba zaidi ya makaburi 20 katika eneo la Mswahili katika kata ya Mkuyuni.

Pamoja na kufukua makaburi, mafuriko hayo yalisababisha hasara kwa wafanyabiashara wa maduka ya jumla na rejareja wa mitaa ya Liberty na Uhuru baada ya bidhaa zao kusombwa na maji ya Mto Mirongo uliokuwa umefurika na kusababisha maji kupita juu ya daraja.

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akitarajiwa kuzungumzia madhara ya mvua hizo leo baada ya kukusanya taarifa kutoka kwa wasaidizi wake, ofisa mtendaji wa Kata ya Mkuyuni, Ibrahim Joseph aliliambia Mwananchi jana kuwa viungo vyote vya binadamu vilivyopatikana sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mkondo wa Mto Kang’anga, imesitiriwa kwa heshima na kufuata imani zote za kidini.

“Tumeshirikiana na ndugu, jamaa, viongozi wa Serikali na vyombo vya dola, waumini na viongozi wa dini kufanya sala na kuhifadhi viungo vyote vya binadamu vilivyofukuliwa na mafuriko,” alisema Joseph.

Makaburi hayo yalifukuliwa baada ya maji mengi kutiririka kutoka maeneo ya milimani na kufanya Mto Kang’anga kufurika hivyo maji kuanza kujitafutia mikondo ambayo mingine ilielekea eneo hilo la makaburi.

Kutwa nzima ya juzi, mtendaji huyo akishirikiana na maofisa wa Jeshi la Polisi, aliwaongoza wakazi wa eneo hilo kufukua mchanga kutoka kwenye mifereji, mitaro, chini ya daraja na makalavati pamoja na mkondo wa Mto Kang’anga kutafuta mabaki ya viungo vya binadamu vilivyofukuliwa kutoka makaburini.

Mzee Hussein Salum (81), ambaye ni miongoni mwa waliozika wapendwa wao katika makaburi hayo, alisema atahamisha kaburi la mke wake, Ashura Idd aliyezikwa eneo hilo mwaka 1997 kutokana na kuwa ukingoni mwa mfereji.

“Sina njia nyingine ya kuokoa kaburi la mke wangu zaidi ya kulihamishia eneo jingine, nikiliacha hapa litafukuliwa kwa sababu liko ukingoni mwa mfereji,” alisema Mzee Salum

Katika tukio jingine, mwili wa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyechukuliwa na maji kutoka mikononi mwa mama yake eneo la Igogo jijini Mwanza, umepatikana.

Ofisa mtendaji wa Kata ya Igogo, Shadrack Mboje aliliambia Mwananchi kuwa mwili wa mtoto huyo ulipatikana juzi eneo la viwandani baada ya kukwama katika chujio maalumu linalochuja maji yanayotiririka kuelekea ziwani.