Mabalozi wa Tanzania ughaibuni watoa neno jengo la ndege Terminal 3

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal three, Injinia Burton Komba akiwaonyesha mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi wakati walipotembelea Uwanja huo leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali wamesema Terminal 3 inaweza kuchochea utalii na uwekezaji katika sekta ya usafiri wa anga, wamesema hayo wakati walipotembelea jengo hilo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Dar es Salaam. Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamesema maboresho yaliyofanywa kwatika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam ni kichocheo cha utalii na uwekezaji katika sekta anga.

Mabalozi hao leo Ijumaa Agosti 16,2019 walitembelea jengo jipya (Terminal 3) katika uwanja huo ili kujionea miundombinu yake, kwa ujumla walifurahia mradi huo ambao ulizinduliwa mwanzoni mwa mwezi huu na Rais wa Tanzania John Magufuli.

Walipofika katika jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia abiria zaidi ya 16,400 kwa siku, walipatiwa maelezo ya jumla ya mradi kisha wakafanya ukaguzi kwa kuingia ndani kama abiria kisha kutoka kama wageni wanaowasili.

Balozi wa Tanzania nchini marekani na Mexico, Wilson Masilingi amesema Watanzania na Wamarekani wanajali mambo ya usalama na viwango na mambo yote hayo yanapatikana katika jengo hilo hivyo wageni kutoka marekani wataongezeka.

“Kazi ya ubalozi kuwakaribisha wageni nyumbani sasa imekuwa ni rahisi kwani mambo yote haya wanayaona katika mtandao, ilikuwa ni aibu kumkaribisha mgeni anaanza kulalamika uwanja wenu umebanana mbona hampanui  lakini hivi sasa nyumbani hapana tofauti na Washington na New York,” amesema Masilingi.

Amesema Wamarekani ambao ni miongoni mwa nchi zinazoleta wageni wengi hapa nchini wanatamani kuwa na safari ya moja kwa moja katika taifa hilo na Tanzania.

“Wanasema wanachoka kuzunguka Ulaya na Mashariki ya kati hii inaweza kuwa fursa kwa shirika letu na soko lilikionekana zuri na mashirika ya kimarekani yatafuata,” amesema

Baraka Luvanda ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini India amesema akirudi huko anakwenda kusambaza taarifa kuwa Dar es Salaam kuna uwanja mkubwa wenye uwezo wa kuhudumia abiria wengi hivyo makampuni yajitokeze yaje kuwekeza huku.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Congo DRC, Paul Meela amesema jengo hilo ambalo kwa sasa linatumiwa na abiria wa safari za kimataifa pekee linatoa taswira ya Tanzania na sasa ni wakati mwafaka wa kuwa na ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Congo.

“Jengo ni zuri sana miundombinu ni mizuri, ni wakati sahihi wa kuanza safari za moja kwa moja kati ya Congo na Tanzania kupitia shirika letu (Air Tanzania), kuna soko kubwa la biashara ya usafiri wa anga kwakuwa kuna Watanzania wengi nchini Congo kuna hata mabasi ya moja kwa moja,” amesema Meela.