Mabalozi wa Tanzania ughaibuni wampongeza Rais Magufuli, ataka wajitathimini

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Alhamisi Agosti 22,2019 amekutana Ikulu ya Dar es Salaam na mabalozi 43 wanaoiwakilisha katika nchi mbalimbali duniani ambapo wametumia fursa hiyo kupongezana na kupeana ujumbe wa kipi kifanyike.

Dar es Salaam. Mabalozi wa Tanzania wanaoiwakilisha katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa nchi hiyo, John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.

Mabalozi hao 43 ambao wapo Tanzania tangu  Agosti 13, 2019 wametoa pongezi hizo leo Alhamisi Agosti,22, 2019 walipokutana na kuzungumza na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya miradi waliyoitembelea mabalozi hao ni ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nojuma.

Pia, walitembelea Zanzibar katika ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi na ujenzi wa barabara ya Kaskazini - Bububu – Mkokotoni .

Mabalozi hao wameeleza utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza baada ya kuwasikiliza Mabalozi hao, Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha nchi na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.

Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.

“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” amesema Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc)

Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.

“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Rais Magufuli.

Kuhusu changamoto mbalimbali walizomueleza, Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishughulikia pale ambapo wao wenyewe wana uwezo na amemtaka Wizara ya Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi kufanyia kazi taarifa wanazopelekewa na Mabalozi  hao kwa wakati.