VIDEO: Mabasi kutoka Dar kuelekea Kagera, Kigoma na Katavi mwiko kusafiri saa 24

Friday August 2 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Liberatus Sabas amesema mabasi yanayotoka  Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi hayataruhusiwa kutembea saa 24 kutokana na sababu za kiusalama.

Kamishna Sabas amesema zuio hilo litahusu pia mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea wilaya mbalimbali za mkoani Tabora ambayo yatalazimika kusimama Tabora Mjini na baadaye kuendelea na safari wilayani.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 2, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wa polisi, hali ya usalama.

Amesema  mabasi yanayotoka mikoa ya Kagera, Katavi, Kigoma kwenda Dar es Salaam yataruhusiwa kutembea saa 24 kama kawaida kutokana na eneo la Morogoro na Dar es Salaam kuwa salama wakati wote.

"Mabasi haya yalikuwa yakitoka kwenye mikoa hiyo yalikuwa yanalala Morogoro, lakini kutokana na hali nzuri ya kiusalama yataendelea na safari hadi Dar es Salaam," amesema Kamishna Sabas.

Amesema mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea katika mikoa hiyo yatalazimika kulala wilayani Kahama kisha kuendelea na safari.

Advertisement

Advertisement