Mabasi yanayoingia, kutoka Dodoma kupuliziwa dawa

Muktasari:

Ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona ambao umewaathiri watu 13 nchini Tanzania hadi sasa, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi ameagiza kupigwa kwa dawa ya kuuwa wadudu kwa mabasi yanayoingia na kutoka jijini humo.

Dodoma. Mkuu wa Wilaya (DC) ya Dodoma Mjini nchini Tanzania Patrobas Katambi ameagiza mabasi yote yanayoingia jijini humo kupigwa dawa za kuuwa wadudu ikiwa ni hatua ya kukakibiliana na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 27 2020, Katambi amewaagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Dodoma Mjini na halmashauri ya jiji kuhakikisha mabasi yote yanayokwenda mikoani kupigwa dawa ya kuuwa wadudu kabla na baada ya safari.

Ameagiza pia kupigwa dawa kwa maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

“Tutafute dawa na tuweze kunyunyuzia dawa (fumigation) wataalam wetu wa afya watatuelekeza ni dawa zipi tunaweza kupiga kwenye maeneo mikusanyiko ya watu wengi au yenye usafiri. Ni wajibu wa taasisi zote lazima tuwe na ndoo zenye maji safi na salama na sabuni,” amesema.

Amesema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya itapita kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha kwenye maeneo yenye watu wengi kama hospitali, vituo vya afya, zahanati, ofisi, maduka, yanawekwa vitakasa mikono (sanitizer).

Amewataka wakazi wa Dodoma kufuata masharti yaliyotolewa na wataalam wa afya ili kuepukana na ugonjwa huo.