Machungu ya laini za simu kuzimwa

Muktasari:

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA idadi ya watumiaji wa simu hadi Septemba, 2019 ilikuwa ni watu milioni 44,798,361, watu 23,692,806 walikuwa wamejiunga na huduma za miamala ya simu, idadi ya miamala iliyokuwa ikifanyika kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2019 ilikuwa ni 252,369,669 huku thamani ya miamala hiyo ikitajwa kufikia Sh8.8 bilioni. TCRA ilitoa tangazo la kuwataka wale ambao tayari wameshasajili laini zao kwa mfumo wa alama za vidole, kuhakiki usajili wao huo kwa kupiga *106# kabla ya TCRA kuzima laini zisizosajiliwa.

Moshi/Dar Usajili wa laini za simu kwa alama za vidole umeingia saa za lala salama huku kukiwa na hofu ya mamilioni ya laini zisizosajiliwa kuzimwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wachumi, wafanyabiashara na mawakala wa miamala ya fedha wametaja athari zitakazotokea baada ya laini hizo kuzimwa keshokutwa Jumatatu.

Mawakala wa fedha wa kampuni kubwa za simu kama Vodacom, Airtel, Tigo, Halotel na wa mitandao mingine, wameingiwa hofu kuwa kuzimwa kwa laini hizo kutaporomosha kamisheni yao.

TCRA ilikuwa imeweka muda hadi Desemba 31 mwaka jana laini zote ziwe zimesajiliwa kwa mfumo huo, vinginevyo zingezimwa.

Hata hivyo, kutokana na wingi wa watu wanaotafuta kitambulisho cha taifa ambacho ndicho kigezo pekee cha kukubalika kusajiliwa, Rais John Magufuli aliongeza muda huo wa siku 20 zaidi kuanzia Januari mosi hadi 20.

Pamoja na nyongeza hiyo ya muda, lakini ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) nchi nzima kumeshuhudiwa foleni isiyo ya kawaida ya wanaohitaji vitambulisho au namba tu ya kitambulisho.

Kwa mujibu wa TCRA, tangu kuanza kwa usajili huo Mei mwaka jana hadi kufikia Januari 12, laini za simu zilizokuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole ni milioni 26 kati ya laini milioni 48 zilizosajiliwa kawaida na kutambuliwa na mamlaka hiyo.

Kutokana na maeneo mengi nchini wananchi kusotea kupata vitambulisho au namba, kumekuwa na maagizo mbalimbali yaliyotolewa na viongozi wa Serikali kwenda Nida akiwamo Rais Magufuli.

Maagizo hayo yalilenga kuwataka Nida kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi ili waweze kupata vitambulisho au namba za utambulisho. Hata hivyo, katika ofisi za Nida kote nchini, kumekuwa na foleni kubwa ya wananchi kuhitaji huduma hiyo.

Baadhi ya maeneo wamemwomba Rais Magufuli kuingilia kati ili kuongeza muda zaidi kwani inaonekana Nida kuelemewa.

Athari zenyewe

Wachumi na wafanyabiashara, wameainisha athari zitakazolikumba taifa kutokana na kuzimwa kwa laini za simu zisizosajiliwa ikiwa ni pamoja na pia kugusa miamala ya kodi za Serikali.

Taasisi nyingi za Serikali na mashirika ya umma zinatumia mfumo wa malipo ya Serikali unaoujulikana kama Government e-Payment Gateway (GePG) unaotumia pia simu za mikononi.

Mbali na Serikali zitapata athari kwa kiasi fulani katika ukusanyaji mapato kwa taasisi zake kama TRA, Mifuko ya Jamii, malipo ya maji na umeme lakini endapo laini hizo zitazimwa zitaathiri huduma za kifedha katika mabenki (sim banking) kwenda kwenye simu na simu kwenda benki.

Lakini ukiacha malipo hayo ya benki kwenda kwenye simu na simu kwenda benki, lakini pia uzimaji utatikisa miamala ya fedha kupitia kwa mawakala wa kampuni mbalimbali za simu.

Halikadhalika wale watakaozimiwa simu watashindwa kufanya miamala ya malipo kwa matumizi wanayoyafanya ikiwamo kulipia ving’amuzi na ununuzi za bidhaa mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Pia, kuzimwa kwa simu hizo kutaathiri mawasiliano ya kawaida ya upigaji simu kutoka mtu mmoja kwenda mwingine na itakuwa na athari hasa vijijini ambako baadhi ya wazazi hawajajisajili.

Lakini athari nyingine itakuwa kwa kundi kubwa la watumiaji wa mtandao wa intaneti watapungua wakijumuisha wanaotembelea tovuti na kuwasiliana kwa mitandao ya kijamii.

Athari nyingine itakuwa kwa ajira binafsi ambazo baadhi wamejiajiri kama kuchajisha simu vijijini na kwenye vituo vya mabasi na maeneo ya biashara, kuwa mawakala wa mitandao ya simu. Hawa wataathirika kwani wateja hawatokuwapo kutokana na upungufu wa wahitaji.

Mtazamo wa wachumi

Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema kuzimwa kwa simu hizo kutaathiri mawasiliano na kuathiri shughuli za kiuchumi.

“Mawasiliano yatakatika na kuathiri shughuli za uchumi na biashara. Mapato ya watu binafsi, makampuni na Serikali yatashuka na pia kupatikana na kufikiwa kwa huduma za kifedha kutashuka,” alisema.

Naye mtaalamu wa masuala ya Fedha nchini, Bosco Simba alisema mawasiliano ya kijamii na kibiashara yaliyokuwapo kati ya wadau mbalimbali yatapotea na kuweza kuleta hasara.

“Simu hutumika kama njia kuu ya malipo ya miamala mbalimbali hivyo itaathirika kwa kufungiwa na fedha zikazuiliwa. Kampuni za simu na Serikali itapoteza mapato kwa wateja kutoweza kufanya mawasiliano,” alisema.

“Zikizimwa itakatisha wateja tamaa na wanaweza wakazoea hali na kuto `renew’ (kutokuhuisha) laini zao mapema kwani tatizo kubwa limetokana na kutopata vitambulisho vya Nida kwa wakati. Serikali iliangalie hili na ije na suluhisho,” alisema Simba.

Mtaalamu mwandamizi wa uchumi kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kiyondo alisema kama watu wote hawatafanikiwa kukamilisha usajili wa alama za vidole kutakuwa na athari kubwa ya kiuchumi kwa kuzingatia mnyororo wa thamani wa huduma za simu.

Alisema athari hazitakuwa kwa mmiliki wa simu pekee bali watu wote waliokuwa wakitegemea huduma za simu kama chanzo za mapato au msaada wa kuwawezesha kujiinua kiuchumi.

“Simu zinatoa huduma za kifedha kwa wengi tofauti na benki ambazo si kila mtu angeweza kuzipata, watu wanaweka akiba, mikopo na kufanya miamala ya kibiashara na huduma lakini pia kuna watoa huduma za simu hivyo watumiaji wakipungua ajira nyingi zitapotea,” alisema.

Wafanyabiashara, mawakala

Mfanyabiashara wa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na mmoja wa mawakala wakubwa wa miamala ya fedha, Patrick Boisafi, alisema jana kuzimwa kwa laini kutakuwa na athari kubwa kiuchumi.

Boisafi ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA ) mkoani Kilimanjaro, alisema athari za kimapato haziepukiki.

“Unajua tatizo kubwa la Watanzania wanapenda kufanya mambo dakika za majeruhi. Sasa kwa hili kwa kweli walichemsha maana bila kitambulisho cha Nida huwezi kusajili simu,”alisema Boisafi.

“Tatizo liko zaidi Nida maana kwenye makampuni ya simu hakuna foleni, lakini ili uende huko lazima uwe na kitambulisho cha Taifa. Wengine simu ndio benki yake, itakuwaje?” Alihoji Boisafi.

Boisafi alisema kwamba kuzimwa kwa simu kutawafanya wale wenye akiba katika simu zao kupotea na uwezekano wa kupata kitambulisho au namba ndani ya miezi mitatu inaonekana haiwezekani.

Wakala, Upendo Mosha anayemiliki pia duka la vipodozi alisema kwamba laini zitakazozimwa zitaleta athari ya kimapato si kwa Serikali tu bali hata kwa mawakala kwa vile hulipwa kamisheni.

“Unajua katika eneo ambalo Serikali inavuna kodi ya uhakika ni kwenye miamala hii ya fedha sasa fikiria kama tukisema asilimia 40 ya laini zinazimwa inakuwaje? Kuna mahali tumekwama,” alisema.

Muuza samaki maarufu katika soko la Manyema mjini Moshi, Ramadhan Besha, alisema ameshawataarifu wateja wake kutomtumia fedha za malipo kupitia simu hiyo kwa kuwa hana uhakika kama ataweza kuisajili hadi kufikia Jumatatu.

“Nimehangaika hapo Nida mpaka nimechoka. Sijapata namba ili nisajili na hii laini ndio kila kitu. Nina wateja wa oda nawatumia samaki halafu baada ya muda wananilipa. Imebidi niwaambie wasitume kwenye laini yangu,” alisema.

Alichokiona CAG

Wakati wananchi wakiendelea kusotea vitambulisho vya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini, kitabu cha Toleo Maalum la Mwananchi la ripoti za CAG kwa mwaka 2017/2018 kilichosainiwa na CAG, Charles Kichere kimeonyesha upungufu uliokuwapo na kutoa mapendekezo ya nini cha kufanya.

Katika taarifa hiyo, CAG Kichere aliainisha upungufu katika utengenezaji wa vitambulisho vya Taifa ambapo aliitaka Nida iharakishe kazi ya usajili na utengenezaji wa vitambulisho hivyo.

Taarifa hiyo ya ukaguzi kwa Serikali Kuu ilibainisha kati ya watu 19,662,105, ni watu 4,511,809 ambao vitambulisho vyao vilitengenezwa chini ya kampuni ya IRIS Corporation Berhard ya nchini Malaysia.

Vitambulisho vilivyotengenezwa ilikuwa ni asilimia 23 tu ya watu waliokuwa wamejisajili na ugonjwa huo unaonekana kuendelea kuitafuna Nida hadi usajili wa simu kwa alama za vidole unapofikia kikomo Januari 20.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya CAG ilisema kampuni hiyo ilikuwa imesimamisha shughuli zake zote za utengenezaji vitambulisho kuanzia Machi 14 mwaka 2018 kwa kutokulipwa deni la Sh69.98 bilioni.

Kutokana na kampuni hiyo kusimamisha shughuli zake, CAG alitoa mapendekezo akiitaka Nida, “iharakishe zoezi la usajili na utengenezaji wa vitambulisho vya Taifa . Pia, itathmini utendaji kazi wa mkandarasi ili kuweza kuamua iwapo imuongezee muda wa mkataba au iingie makubaliano na mkandarasi mwingine.”

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janeth Joseph (Mosi) na Ephrahim Bahemu (Dar)