Madai ya uchochezi chanzo Mbowe kukamatwa

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamdun amesema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekamatwa na polisi baada ya kutoa maneno ya uchochezi.

Moshi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamdun amesema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekamatwa na polisi baada ya kutoa maneno ya uchochezi.

Amesema kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa maneno hayo leo Ijumaa Februari 28, 2020 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Nkoromu Masama kati wilayani Hai.

Amebainisha kuwa maneno aliyoyatoa mbunge huyo wa Hai yanaashiria  uchochezi  na kuamsha hisia za wananchi na chuki dhidi ya Serikali ya Tanzania na polisi.

"Mbowe amekamatwa na anashikiliwa na polisi baada ya kutuhumiwa kusema au kutoa maneno yanayoashiria uchochezi, kuamsha hisia na chuki dhidi ya Serikali na polisi. Anahojiwa lakini baada ya mahojiano atapewa haki ya dhamana,” amesema kamanda Hamdun.

Katika mkutano huo,  Mbowe amesema hawezi kupongeza utendaji kazi wa Serikali mpaka atakapokuwa na uhakika Serikali inatenda haki kwa watu wote.

Alikamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara saa 11:58 jioni.

Wakati akijiandaa kuondoka eneo hilo, polisi walikwenda katika gari lake wakieleza kuwa wanamhitaji kituoni, ombi ambalo liliridhiwa na mwenyekiti huyo wa Chadema baada ya mvutano uliodumu takribani robo saa.

Awali, akizungumza katika mkutano huo Mbowe amesema licha ya kupitia  kipindi kigumu na changamoto mbalimbali za kisiasa, hawezi kukoma kuendelea na mapambano.

Huku akisisitiza kuwa hajawahi kupitia kipindi kigumu katika siasa kama sasa Mbowe amesema, “kufa sijafa lakini cha mtemakuni nimekiona, nimekaa jela, mahabusu na mahakamani nimekwenda lakini sikomi ng'o, ndio kwanza wananitia moto.”

Amesema haogopi kufa wala kwenda jela, huku akigusia umuhimu wa kujenga miundombinu ya barabara na reli na kuwaacha wananchi kuwa huru.

"Hakuna kitu chenye thamani katika maisha yenu kama uhuru wenu, mkijengewa barabara, shule lakini mkanyimwa uhuru wenu ni bora mvikose hivyo vyote lakini mpate uhuru wenu na hayo ndiyo maneno ambayo Chadema tumehubiri,” amesema Mbowe.

Mbunge huyo wa Hai amesema wananchi wanahitaji nchi ya demokrasia, wote walindwe, “mkiwa Chadema mlindwe, CCM nao walindwe, kila mmoja katika nchi hii ajione kuwa ni raia mwenye haki na awe na uhuru.”

Amesema wanahitaji askari walinde mikutano kwa amani na wananchi waone raha ya kwenda kwenye mikutano, na si kuwajaza hofu.

Aliwaondoa hofu wananchi kutokana na kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba hata kama atafungwa, akitoka mapambano yataendelea.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amewaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa amemuandikia barua Rais John Magufuli  kutaka uchaguzi wa Serikali za mitaa urudiwe nchi nzima.

“nimemuandikia Rais barua nimemwambia Chadema kama chama kikuu cha upinzani hawawatambui wenyeviti wa Serikali za mitaa waliochaguliwa, tunahitaji  uchaguzi urudiwe nchi nzima ili wapatikane viongozi waliochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi,” amesema Mbowe.

Mbowe leo ndio ameanza ziara ya siku tano katika jimbo la Hai inayoambatana na mikutano ya hadhara, na amebainisha kuwa kesho Februari 29, 2020 atazungumza mapema na wananchi wa eneo la Bomang'ombe.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi