Madiwani waliojiuzulu CUF, washiriki mkutano baraza la jiji Tanga, wapitisha bajeti

Meya wa Jiji la Tanga Mhina Mustapher (Selebos)akiendesha kikao cha baraza la madiwani kilichofanyioka jana ambacho Naibu Meya wa Jijila Tanga,Mohamed Haniu (kushoto) ni miongoni mwa madiwani nane waliohama
CUF na kuhamia CCM akiwa katika kikao hicho  na kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga,Daud Mayeji.Picha zote na Paskal Mbunga

Tanga. Siku 11 kupita tangu madiwani wanane wa CUF jijini Tanga kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na CCM wameibuka na kushiriki kama wajumbe halali wa baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji hilo na kupitisha bajeti ya Sh66.1 bilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.

Hatua hiyo imezua mjadala kwa baadhi ya wadau kudai madiwani hao hawakupaswa kushiriki kikao hicho baada ya kutangaza hadharani kuhama chama chao ina maana walikuwa wamejivua nyadhifa zao.

Hata hivyo sintofahamu imeibuka baada ya uongozi wa jiji la Tanga kudai kuwatambua madiwani hao wakati chama chao kimewakana.

Madiwani hao ambao walijizulu na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, Januari 15, mwaka huu akiwa ziarani mkoani Tanga, jana waliingia katika ukumbi wa mkutano wakiwa wamevalia majoho ya wajumbe wa kikao hicho.

Madiwani hao waliojiondoa CUF wakiongozwa na naibu meya, Mohamed Haniu ni; Mswahili Njama (Chongoleani), Said Alei (Masiwani), Nassoro Mohamed (Tongoni), Habib Mpa (Ngamiani kati), Hidaya Ahmed, Sureha Mahadhi na Mwanasha Abdallah (wote viti maalum).

Wakati Dk Bashiru akiwapokea wanachama hao, alisema mwanachama anayejiunga CCM wakati huu ana haki sawa na mwanachama wa muda mrefu.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daud Mayeji kujua uhalali wa madiwani hao kushiriki kikao hicho, alisema hana taarifa za madiwani hao kujiuzulu na kujiunga na CCM.

“Mimi naendesha ofisi hii kwa kufuata sheria na ndiyo zinazoniongoza.

“Kila chama kinatambua mwanachama wake anapohama ni lazima niletewe barua ya kunitaarifu ili niweze kuingiza taarifa hizo kwenye kumbukumbu kwa mujibu wa taratibu, sasa sijui kama hao wa CUF wamehama, maana sina taarifa ya maandishi” alieleza Mayeji.

Naye Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alidai hana taarifa za kikao hicho na ushiriki wa madiwani hao na kuahidi kufuatilia kujua undani wake.

“Hatuna taarifa ya kikao cha baraza la madiwani wa jiji la Tanga ili nitajua taarifa zikija mezani,” alieleza Waitara.

Naye Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustpaha alisema anatambua madiwani hao ni halali na kutaka aliye na hofu na hilo amuwasilishie barua inayoonyesha wamehama chama chao na kuhamia CCM.

Wakati huo huo, Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo, Udhibiti na Utafiti, Masoud Omari alisema kisheria bajeti iliyopitishwa katika kikao hicho ni batili kwa sababu kimehudhuriwa na wajumbe wasio halali. “ Huu ni uvunjaji wa sheria, kanuni na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Masoud.

Alisema kutokana na tukio hilo, CUF Taifa inawasiliana na wanasheria wake ili kumfikisha mahakamani Mkurugenzi wa jiji la Tanga, Mayeja.

“Mkurugenzi kisheria ndiye anayethibitisha akidi ya kikao, alipoona madiwani waliohama CUF wakiwa kwenye viti vyao vya awali na wamevaa majoho kama wajumbe halali alitakiwa kushauri waende wakakae viti vya waalikwa na wasihusike na maamuzi yoyote” alisema Masoud.