UDHIBITI WA MAKADA NDANI YA CCM: Maelezo ya Membe yaacha maswali

Dar es Salaam. Bernard Membe alitarajiwa kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM akiwa mnyonge, asiyetaka kuzungumzia kilichojiri na mwenye kutafakari mustakabali wake, lakini alikuwa tofauti; alitoka kikaoni akionekana jasiri, mcheshi na mwenye uhakika.

Hakutaka kuingia kwa undani kuelezea walichozungumza, badala yake alizungumzia mambo hayo kiumjula; kuhusu CCM, masuala ya kitaifa, kimataifa na fursa aliyopata kutoa maoni yake.

Lakini kikubwa ni maswali yanayoibuka kutokana na maelezo mafupi aliyotoa baada ya kikao hicho akiwa amekaa ndani ya gari yake aina ya Range Rover nje ya jengo la makao makuu ya CCM, maarufu kwa jina la White House, jijini Dodoma.

Membe, ambaye amekuwa na mgogoro na chama hicho tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliitwa na kamati hiyo kuhojiwa kuhusu sauti zilizoenea katika mitandao ya kijamii zinazomhusisha yeye pamoja na January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Mazingira na Muungano, Nape Nnauye (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) na William Ngeleja, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Wengine ni makatibu wa zamani wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba ambao pia wameitwa kujieleza mbele ya kamati hiyo.

Katika sauti hizo, makada hao wa CCM wanasikika wakizungumzia kuporomoka kwa chama hicho kikongwe, uendeshaji mbovu wa nchi na pia kumlaumu mwenyekiti ambaye ndiye Rais wa Tanzania.

Membe alithibitisha kuwa sauti moja inayosikika katika mikanda hiyo ni yake, wakati Ngeleja, Nape na Makamba walikwenda Ikulu kuomba radhi kwa Rais John Magufuli.

Inaonekana Membe anasimamia kauli yake na ilipotolewa taarifa kuwa wameitwa kuhojiwa, alifurahia kupata nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu kile anachoamini na amedhihirisha hilo juzi.

“Tulikuwa na mkutano wa saa tano na mijadala mizuri, mikubwa ya kitaifa inayohusu CCM na nchi yetu,” alisema Membe, mmoja wa makada 38 wa chama hicho waliojitokeza kuomba ridhaa ya kupitishwa kugombea urais mwaka 2015.

“Nimekuwa mtu wa furaha kubwa ajabu kwa sababu nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa.

“Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu kilitaka kuyajua. Nimepata nafasi nzuri ya kutoa mawazo ya yale mambo ambayo niliombwa kutoa mawazo.

“Hivi sasa mimi na mke wangu tunakwenda kula chakula kizuri sana katika hoteli moja ambayo haijulikani na baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam.”

Lakini muhtasari alioutoa juzi kuhusu mahojiano hayo, hauonekani kuwa ndio mwisho kwake kuzungumzia suala hilo.

“Ninawaambia tu safari ya kuja Dodoma ilikuwa ya manufaa makubwa sana kwangu, kwa chama na kwa Taifa letu. Mengine yatakuwa yakipatikana kidogokidogo nikishiba,” alisema huku akitabasamu.

Mazungumzo katika sauti hizo zilizosambaa mitandaoni yamejikita katika kuzorota kwa chama, lakini waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, alidokeza kuwa walizungumza pia masuala ya kitaifa na kimataifa.

Haijaeleweka sababu za kuzungumzia masuala ya kimataifa wakati wakimhoji kuhusu nidhamu yake katika chama, lakini katika mahojiano maalum na Mwananchi mwaka 2015, Membe alikosoa mkakati wa Rais John Magufuli wa kubana matumizi kwa kudhibiti safari za nje ili mabalozi wafanye kazi hizo.

‘Ukijitenga, utatengwa’

Alisema Rais Magufuli ni lazima ataenda nje hata kama amejiwekea utaratibu wa kutosafiri.

“Utaenda mwenyewe au mawaziri wako na hasa Waziri wa Mambo ya Nje kwa sababu kuna vikao nje ya nchi ambavyo mabalozi hawaruhusiwi kuingia,” alisema Membe wakati huo.

“Ukijaribu kujifanya kisiwa utakuwa kama Zimbabwe. If you isolate yourself you will be isolated (kama ukijitenga, utatengwa).”

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje ni lazima asafiri nje na kwamba “ukiona hasafiri, ujue mgonjwa”.

Kuhusu mahojiano hayo kuhusisha masuala ya kimataifa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) anasema ilikuwa sahihi.

“Aliitwa kwa kuwa alizungumzia chama, kudaiwa anamsaliti Magufuli kwa kutaka kugombea,” alisema Profesa Mpangala.

“Kwa hilo, lazima atoe ufafanuzi. Pengine kueleza masuala ya sera ya chama, huenda ndio maana akasema suala la kimataifa maana anaweza kuwa amesema kuhusu jumuiya za kimataifa zinavyoitazama Tanzania. Hiyo ni ndani kabisa ya mada ambayo ameitiwa, ni kama ametoa ufafanuzi kwa nini anaikosoa Serikali.”

Amesema hayo wakati Tanzania ikifanya jitihada za kurekebisha uhusiano mazuri na baadhi ya taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya na nchi kama Marekani, ambayo kwa mara ya kwanza imezuia raia wa Tanzania kuingia katika bahati nasibu ya kupata uraia wake.

Benki ya Dunia imesimamisha mkopo wa dola 500 milioni za Kimarekani (sawa na Sh1.2 trilioni) kutokana na kutotekelezwa kwa masuala ya kijamii na kisiasa, wakati EU imeteua balozi mpya baada ya aliyekuwepo kurejeshwa nyumbani. Sweden imepunguza kiwango cha misaada.

Suala jingine lililoibua maswali ni dokezo kwamba walijadili masuala ya kitaifa.

Ingawa kuzungumzia uongozi wa chama hicho ni kuzungumzia mustakabali wa Taifa kwa kuwa ndicho kilichoshika hatamu kwa sasa, Membe hakuweka bayana masuala hayo.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi mwaka 2015, aligusia dosari katika mambo ambayo Rais Magufuli alikuwa ameanza kuyafanya, kama kushughulikia wafanyabiashara waliokuwa wanakwepa kodi.

Katika mahojiano hayo ya mwaka 2015, Membe alisifu jitihada za kukusanya kodi, akisema duniani hakuna nchi inayoendelea bila ya kodi, lakini akasema ni lazima Rais alifanye kwa uangalifu mkubwa ili asiwafukuze wawekezaji ambao kimsingi ndiyo wabia wa maendeleo ya taifa.

“Wafanyabiashara ni watu wa kuwa-handle (kushughulika nao) vizuri na kwa uangalifu mkubwa kwa sababu wao ndio gurudumu la maendeleo ya nchi yoyote duniani,” alisema.

“Tunapozungumzia ajira unawazungumzia wafanyabiashara ambao ndio wawekezaji, sasa ombi langu ni kwamba Serikali isicheze nao.

(Wafanyabiashara) Ni kama ndege ambaye ili uendelee kuwa naye lazima umshikilie hivi (akionyesha ishara), lakini ukiachia vidole atarudi na kwenda kutaga mahali kwingineko.”

Bila ya kufafanua, Membe alisema “si dhambi kwa wafanyabiashara kufadhili vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, lakini akishapatikana Rais, Serikali ina wajibu wa kuwakusanya wafanyabiashara wote na kufanya nao kazi ya ujenzi wa taifa na si kuwaburuza”.

Mbunge huyo wa zamani wa Mtama alisema wafanyabiashara wana masikitiko dhidi ya Serikali na alibashiri kuwa suala hilo lingeibuka bungeni.

Wakati huo, wafanyabiashara waliobainika kukwepa kodi walipewa siku chache walipe, lakini Membe alikosoa akisema “ingekuwa mimi sikupi siku tatu wala siku saba kulipa kodi hiyo. Nakupa miezi miwili mpaka mitatu ili uweke sawa mahesabu yako kwa sababu kutunza hesabu si jambo rahisi na baada ya hapo nitakwambia tuendelee kuijenga nchi pamoja”.

Suala jingine la kitaifa alilodokeza ni wimbi la kutumbua watendaji wakuu wa taasisi za Serikali na watumishi wa umma kwa sababu tofauti, zikiwemo ufisadi na uzembe.

“Ni rahisi kumshughulikia mtu usiyemfahamu, lakini si rahisi kumshughulikia unayemfahamu,” alisema Membe.

“Kwake kufanya hivyo ni rahisi kwa kuwa pia ni rahisi kuwashughulikia watu usiowajua kuliko watu unaowajua. Lakini hebu tuone kama atafanya hivyo pia kwa hao aliowateua mwenyewe.”

Uchaguzi Zanzibar

Pia Zanzibar ni jambo jingine la kitaifa ambalo Membe alizungumzia, akisema kilichotokea kiliishtua dunia. Uchaguzi huo ulifutwa katika hatua ya kutangazwa kwa matokeo ya rais. Baada ya miezi mitatu uliitishwa uchaguzi mwingine na CUF ilisusia.

“Watanzania waelewe, kilichoishitua dunia ni kule kufuta matokeo kwa ujumla wake (wa rais na wawakilishi). Yaani majimbo yote hakuna hata moja lililofanya vizuri?” Alihoji.

“Hapa ndipo tunapata kigugumizi. Sasa tunakwenda wapi? Tunafanya kitu gani? Ilitakiwa kuwe na ubaguzi, majimbo mawili; matatu, manne, matano, haya hayajafanya vizuri ndiyo uchaguzi urudiwe.

Kaubaguzi kale kangewekwa. Hiyo inafanana na sura ya dunia ya haki.”

Alisema anayedhani tatizo la Zanzibar litamalizwa na sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee, anafanya makosa makubwa.

“Umoja wetu na Zanzibar ni umoja wa kusaidiana wakati wa raha na matatizo. Hili ni tatizo ambalo linaweza kuhatarisha si tu usalama wa Zanzibar bali pia Muungano wetu,” alisema na kushauri CCM na Serikali zishiriki kumaliza mgogoro huo.

Pia swali jingine ni “furaha” aliyopata baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, ambayo iliwahi kumsimamisha yeye pamoja na makada wengine watano kujihusisha na uchaguzi ndani ya CCM.