Mafuriko yazoa daraja, wananchi wahaha kusaka huduma muhimu

Friday February 14 2020

By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro zimesababisha daraja linalounganisha kijiji cha Ndole na maeneo mengine kukatika jambo lililosababisha usumbufu kwa wananchi.

Hali hiyo imesababisha wakazi wa kijiji hicho kilichopo kata ya Kanga wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro kulazimika kuvuka kwa kutumia daraja la muda lililojengwa kwa miti.

Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Februari 14, 2020 mkazi wa kijiji hicho, Ivni Mlambali amesema hali hiyo imesababisha washindwe kupeleka bidhaa zao sokoni pamoja na kushindwa kuzifikia huduma nyingine muhimu.

Halima Issa, amesema wamekuwa wakipata huduma ya afya katika vijiji jirani ambavyo ili wafike ni lazima wavuke eneo hilo.

“Sasa hata watoto wetu wanashindwa kwenda shule kwa kuwa shule ya Msingi Ndole ipo upande wa pili, tunaiomba Serikali iharakishe suala hili,” amesema.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero,  Florent Kyombo amesema amepata taarifa za daraja hilo kusombwa na maji na taarifa zimeshapelekwa kwa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads).

Advertisement

Kaimu meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro,  Godwin Andaluwisye amesema wameshindwa kufanya ujenzi wa daraja jipya kwa wakati kutokana na mvua zinazoendelea.

“Lakini pamoja na eneo hilo kufanyiwa matengenezo ni kwamba tunajenga daraja la kudumu lenye upana wa mita 15, hapa tunapoongea mitambo ipo eneo la tukio na kuna korongo lina maji mengi, mvua zinazonyesha zinasababisha mkandarasi kusimama kwa muda mpaka zitakaposimama,” amesema.

Advertisement