Magereza watahadharisha kuwapo kwa matapeli wa msamaha wa Rais

Sunday December 15 2019

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jeshi la Magereza limetahadharisha kuwepo kwa utapeli kwa baadhi ya watu wasio waaminifu wanaowafuata ndugu na jamaa za wafungwa walioko magerezani na kuwaomba fedha wawasaidie kuwawezesha  ndugu zao kunufaika na msamaha.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Magereza, SSP Amina Kavirondo leo Desemba 15, 2019 kitendo hicho cha utapeli ni kosa la jinai kwani msamaha huo hutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano pekee.

Taarifa hiyo imekuja kufuatia msamaha uliotolewa na wa Tanzania, Rais John Magufuli wakati wa sherehe za Uhuru  Desemba 9, 2019 zilizofanyika kitaifa jijini Mwanza.

“Kitendo hicho ni utapeli na ni kinyume cha Sheria za nchi. Hivyo Jeshi la Magereza linautahadharisha umma wa Watanzania wote kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45 (1) (d)

mwenye mamlaka ya kusamehe wafungwa ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si mtu mwingine yoyote,” amesema SSP Kavirondo.  

 Ameongeza, “Kwa Muktadha huo, mtu yeyote atakaye jitokeza na kudai kuwa anauwezo wa kusaidia ndugu aliyefungwa gerezani kunufaika na msamaha huo apuuzwe kwa kuwa hana mamlaka hayo na taarifa za tukio hilo zitolewe haraka iwezekanavyo katika vyombo vya Sheria ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yake.”

Advertisement

Advertisement