Magufuli: Kama si maboresho Moi, Askofu Ruwa’ichi angekufa

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kama isingekuwa kuboresha vifaa tiba katika Taasisi ya Mifupa (Moi) Askofu Yuda Thadeus Ruwa'ichi ambaye alifanyiwa upasuaji wa kichwa kwenye taasisi hiyo Septemba mwaka jana angepoteza maisha.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema isingekuwa kuboresha vifaa tiba katika Taasisi ya Mifupa (Moi) Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam nchini Tanzania, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa'ichi angepoteza maisha.

Mkuu huyo wa nchi ameyasema hayo leo Alhamisi Febuari 20, 2020 katika mkutano wa madaktari na watumishi wa Sekta ya Afya unaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Askofu Ruwa’ichi alifanyiwa upasuaji wa kichwa katika taasisi ya Moi mwezi Septemba mwaka jana baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi.

Akizungumzia kilichosaidia kuokoa maisha ya Askofu Ruwa’ichi, mkuu huyo wa nchi amesema kama isingekuwa uwepo wa vifaa Moi askofu huyo asingepona.

“Tunahitaji kufanya operesheni mpaka za vichwa, nakumbuka Askofu Ruwa’ichi alikuwa apoteze maisha lakini amekuja pale (Moi) mimi sikuamini, lakini hawa hawa watu wakasimamia kazi mpaka akapona yule askofu” amesema Rais Magufuli.

“Ni kwasababu kulikuwa na vifaa, pasingekuwa na vifaa asingekuwa maishani, huwezi kuajiri madaktari wengi wakati hakuna vifaa,” amesema

Amesema kuwa Serikali inaangalia vipaumbele kwenye hospitali kwa kufuata ushauri wa wataalamu.