Magufuli: Nahisi Wizara ya Mambo ya Ndani ina mapepo - VIDEO

Muktasari:

Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema anahisi Wizara ya Mambo ya Ndani ina mapepo na kumtaka Waziri mpya wa wizara hiyo, George Simbachawene kuwa mkali, kumtanguliza Mungu mbele.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema anahisi Wizara ya Mambo ya Ndani ina mapepo na kumtaka Waziri mpya wa wizara hiyo, George Simbachawene kuwa mkali, kumtanguliza Mungu mbele.

Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 27, 2020 Ikulu, Dar es Salaam baada ya kumuapisha Simbachawene, waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu na mabalozi watatu.

Simbachawene amechukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Awali mbunge huyo wa Kibakwe alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wizara  ambayo kwa sasa inaongozwa na Zungu.

Lugola alivuliwa cheo chake kutokana na sakata la mkataba mbovu wa manunuzi ya vifaa vya uokoaji, huku Thobias Andengenye akivuliwa ukuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuhusika kusaini mkataba huo uliokiuka sheria ya manunuzi na ambao haukupitishwa na Bunge, kwa mujibu wa Rais Magufuli.

Miongoni mwa vifaa vilivyotakiwa kununuliwa ni ndege zinazoruka bila ya rubani na magari kwa ajili ya uzimaji moto na uokoaji.

Katika sakata hilo aliyekuwa kamishna jenerali wa Jeshi la Magereza, Faustine Kasike aliondolewa huku katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu, akiandika barua ya kujiuzulu na kukubaliwa na Magufuli.

Leo Ikulu, Magufuli amemtaka Simbachawene kubadili baadhi ya vitu katika wizara hiyo, kuwaondoa watendaji wasiofaa ili kuboresha utendaji.

“Nimekupeleka katika Wizara ambayo nahisi ina mapepo sasa mapepo hayo yasikuingie uwe mkali, usimamie, naamini utaweza na wakati mwingine umtangulize Mungu,” amesema Magufuli.

Amesema licha ya Simbachawene kupelekwa wizara ngumu, ugumu huo anaweza kuuleta mwenyewe.

“Na mawaziri wote huwa nawaeleza lakini sifahamu huwa kuna mdudu gani pale, sifahamu sasa nataka nikupeleke wewe sijui ni mgogo sijui ni mhehe nenda kayasimamie,” amesema Magufuli.

Amewataka watendaji serikalini kutoingia mikataba bila kuihusisha wizara ya Fedha na Mipango.

 “Hili la mkataba tumeshawaachia watu wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) sijui kama watafanya kazi vizuri au wataanza kuogopa ila nina uhakika hili watalifanyia kazi bila kujali nafasi za watu ili rasilimali hii ndogo iweze kutumika vizuri kwa ajili ya manufaa ya watu,” amesema.

Alimtahadharisha Simbachawene kuwa watendaji wote atakaowakuta katika wizara hiyo wanajua kuhusu suala hilo huku akimtaja naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, “lakini (Masauni) hakuhusishwa sana ila alikuwa akipewa nakala ya madokezo na alikuwa ananyamaza hasemi serikalini.”

“Sifahamu kwa nini naye alikaa kimya lakini hakuhusika sana, Naibu katibu mkuu (Wizara ya Mambo ya Ndani) amehusika sana tangu kuanza kwake mpaka mwisho na una watendaji wengine katika Jeshi la Zimamoto wamehusika sana.”

Amesema kupitia mkataba huo, fedha walizokuwa wakilipwa viongozi waliokuwa wakishiriki kikao hicho wangeweza kujiuliza sababu za kupewa kiwango hicho lakini hawakuliona hilo hadi mkataba uliposainiwa.

“Kwa akili za kawaida tu unaweza kuelewa kuna kitu cha ajabu kinafanyika,  kama ni cha kawaida kwa nini ulipwe. Watendaji wako hawakuliona hilo hadi wakasaini mkataba wakapelekwa na nje.”

 “Sasa wewe (Simbachawene) ni mwanasheria nendeni mkaangalie namna ya kumaliza huo mkataba, hayo makubaliano ya kulipa Sh1 trilioni bure, hapana,” amesema Magufuli.

Mabalozi walioapishwa ni Maimuna Tarishi ambaye ni balozi wa Tanzania Umoja wa mataifa Uswisi.

Wengine walioapishwa ni Hussein Katanga (Japan), Profesa Kennedy Gaston (Marekani- New York).