Magufuli: Sitaki CCM iwategemee matajiri - VIDEO

Muktasari:

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli  amesema katika uongozi wake hataki kuona chama hicho tawala nchini Tanzania kinaendelea kuwa ombaomba na kuwategemea matajiri wachache.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli  amesema katika uongozi wake hataki kuona chama hicho tawala nchini Tanzania kinaendelea kuwa ombaomba na kuwategemea matajiri wachache.

Amesema hilo litawezekana endapo watumishi wa chama hicho wataendelea kufanya kazi na kukusanya mapato yanayotokana na miradi ya chama hicho ili waweze kuendesha vyema shughuli za chama.

Amesema  matajiri lengo lao ni kukimiliki chama na kukiweka mifukoni jambo ambalo si zuri kwa maendeleo ya CCM.

Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020  katika mkutano na viongozi wa wilaya ya mikoa wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

“Niwapongeze mnafanya kazi nzuri tukiendelea hivi  mapato ya chama chetu yataendelea kuongezeka kwa kasi na tutaweza kugharamia shughuli mbalimbali ikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu ujao.”

“Hatutaki kuona chama kinaendelea kuwa ombaomba na kuwategemea matajiri wachache ambao baadaye wanajimilikisha chama na kukiwe mifukoni mwao,” amesema Magufuli.

Ameongeza, “nawahakikishia hilo halitatokea kwenye kipindi cha uenyekiti wangu, hiki ni chama cha Watanzania wote na sio kikundi cha watu wachache.”