Magufuli: Uchaguzi umekwisha

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 umekwisha na sasa kinachotakiwa kufanyika ni kujikita katika masuala ya maendeleo

Dar es Salaam. “Uchaguzi umekwisha, uchaguzi umekwisha, uchaguzi umekwisha.”  Ni kauli ya Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyoitoa leo Alhamisi Novemba 5, 2020 katika hotuba yake muda mfupi baada ya kuapishwa na kubainisha kuwa kinachofuata ni kujikita katika maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Magufuli anayeongoza tena nchi kwa mhula wa pili, ameahidi kuendeleza na kukuza ushirikiano na nchi rafiki pamoja na taasisi mbalimbali kama ilivyokuwa katika miaka mitano iliyopita.

Magufuli amesema ili kufanikisha hilo atashirikiana na watu wote kuhakikisha yote aliyoahidi wakati wa kampeni yanatekelezwa.

“Uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha, jukumu kubwa na muhimu lililo mbele yetu  ni kuendeleza jitihada za kulijenga na kuleta maendeleo kwa nchi yetu.”

“Niwahakikishie kuwa kiapo nilichoapa hivi punde na alichoapa Makamu wangu (Samia Suluhu Hassan) tutakienzi kwa nguvu zote, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, dini, kabila au rangi, nitashirikiana nanyi nyote,” amesema Magufuli.

Amesema anakumbuka aliyoahidi katika kampeni atakayetekeleza pamoja na yaliyoandikwa katika Ilani ya chama chake ikiwa ni pamoja na kuendelea  kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, uhuru wa nchi na mipaka yake, muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.

“Nitashirikiana nanyi kwa karibu katika kuendeleza jitihada zetu za kujikomboa na kujenga Taifa litakalojigemea na katika hilo tunalenga kukamilisha miradi mikubwa tuliyoanzisha na kuleta mingine mipya,” amesema.