Magufuli: Vya bure vina madhara yake

Muktasari:

Rais Magufuli amesema kilichosababisha miaka 23 bila kujengwa meli ndani ya ziwa Victoria ni kwa sababu ya kutegemea wafadhili huku akionya kwamba vya bure vina madhara yake.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema licha ya kuahidi kujenga meli mpya wakati wa kampeni zake mwaka 2015, lakini hakujua fedha atazitoa wapi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 8, 2019 wakati akihutubia mamia ya wananchi wakati wa kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Butiama.

“Hata nilipokuwa naahidi sikujua fedha hizi nitazitoa wapi, kumbe fedha zipo zinachezewa na mafisadi, tuliwabana tukazipata hela hizi,” amesema.

Amesema hata sasa bado mafisadi wapo hawajaisha ila wataendelea kuwashughulikia.

Amesema kinachochelewesha maendeleo ni kutegemea misaada na mikopo. “misaada inatuchelewesha mno, siku za nyuma tulifikiri kuombaomba kunatusaidia ndiyo maana miaka 23 tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba haikuwahi kujengwa kwa sababu ya kutegemea misaada,” amesema.

“Siku zote ukisubiri vya bure kupewa vinamadhara yake, sisi sio masikini tujenge tabia ya kujitegemea,” amesema.