Magufuli aagiza mahabusu wanaoshikiliwa kimakosa waachiwe

Rais wa Tanzania, John Magufuli 

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewahutubia wananchi wa Kongwa jijini Dodoma leo Alhamisi na kuzungumzia msongamano wa mahabusu gerezani ambapo ameagiza vyombo vya dola kufuatilia mahabusu wanaoshikiliwa kimakosa kuachiwa huru


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameagiza wizara katiba na Sheria pamoja na vyombo vingine vya ulinzi vinavyohusika na Mahakama wapitie magereza yote nchini huko wakae wazungumze na watuhumiwa waliopo mahabusu ili kubaini mahabusu wote wanaoshikiliwa kimakosa waachiliwe.

Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi Julai 18, 2019 wakati akizungumza na wananchi wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Amesema baada ya kutoa maagizo kwa wizara ya sheria, alipokuwa mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi, maofisa wa wizara hiyo walikwenda katika gereza la Butimba jana Jumatano Julai 17 mwaka 2019 na kukaa na watuhumiwa hao kwa saa saba, ambapo baada ya mazungumzo hayo watuhumiwa mbalimbali waliachiwa.

Aidha Rais Magufuli ameeleza baada ya maofisa wa wizara hiyo kutembelea katika magereza mbalimbali, jumla ya watuhumiwa 300 waliokuwa wanashikiliwa kimakosa wameachiwa huru ambapo katika gereza la Butimba watuhumiwa 75 waliachiwa kutoka mahabusu.

“Wilayani Bariadi wameachiwa watuhumiwa 100, Mugumu Serengeti watuhumiwa 52, Tarime watuhumiwa 6, Bunda watuhumiwa 24 na Kahama watuhumiwa 43 wameachiwa” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameeleza maofisa hao wanaendelea kupitia kila gereza kufanya uhakiki kwa watu wanaoshikiliwa kimakosa waachiwe, na leo Alhamisi maofisa hao watakuwa kwenye gereza la Kasungamile na Geita.

“Siwezi kutawala nchi yenye machozi na watu wanaosikitika kwa unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa,” amesema Rais Magufuli.